Header Ads

Ukanushi wa Habari iliyosambaa mitandaooni kuwa serikali itatoa ajira

SERIKALI YAKANUSHA KUHUSU TAARIFA ZINAZOSAMBAA KUWA ITAANZA KUTOA AJIRA

YAH: KUKANUSHA HABARI ILIYOSAMBAA KATIKA MITANDAO YA KIJAMII IKIMNUKUU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS (MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA) MHESHIMIWA ANGELLAH J. KAIRUKI (MB), KUWA SERIKALI ITAANZA KUTOA AJIRA, KUPANDISHA VYEO NA KULIPA STAHIKI MBALIMBALI ZA WATUMISHI WA UMMA MWEZI FEBRUARI, 2017.

1. Ipo taarifa inayosambaa katika mitandao ya kijamii ikimnukuu Waziri wa Nchi -Ofisi ya Rais (Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora) Mhe. Angellah J. Kairuki (Mb), kuwa Serikali itaanza kutoa ajira, kupandisha Vyeo na kulipa Stahiki mbalimbali za Watumishi wa Umma mwezi Februari, 2017. Chanzo cha habari hiyo ni mtandao wa Jamii Forum kupitia mjadala ulioanzishwa na nkanga chief (JF-Expert Member) na baadaye kusambazwa katika mitandao mingine.

2. Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora inapenda kuwafahamisha Watumishi wa Umma na Umma kwa ujumla kuwa, taarifa hiyo haina ukweli wowote na ina lengo la kuupotosha Umma. Hivyo watumishi wa umma na wananchi kwa ujumla wanaombwa kuipuuza taarifa hiyo na kuendelea na majukumu yao kama kawaida.

3. Serikali inasisitiza kuwa, suala la Ajira mpya na upandishaji Vyeo litafanyika kwa kuzingatia Bajeti ya Serikali ya Mwaka wa Fedha

 2016/17. Malipo ya stahili za watumishi wa umma yatafanywa na Serikali kwa kuzingatia, Sheria, Kanuni na Taratibu zilizopo.

4. Ikumbukwe, Serikali ina utaratibu maalum wa kutoa taarifa kwa Umma, hivyo Serikali itatoa taarifa rasmi kwa Umma kupitia mamlaka husika.

5. Serikali kupitia taarifa hii inawaasa wananchi kuacha tabia ya kusambaza habari za uongo au zisizothibitishwa dhidi yake. Serikali haitasita kuwachukulia hatua za kisheria wale wote watakaobainika kuzusha na kusambaza habari za upotoshaji kuhusu shughuli za Serikali.

Imetolewa na:

Florence Temba

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,

Ofisi ya Rais (Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora)

24 Oktoba, 2016

Share

View web version

Powered blogger
 

About | Contact | Disclaimer | Privacy Policy |Sitemap

   Hata Habari zenye uhakika 

No comments

Powered by Blogger.