MAJARIBIO YA CHANJO YA KWANZA YA MALARIA DUNIANI YAONYESHA MAFANIKIO
Majaribio ya
chanjo ya ugonjwa wa malaria yameonyesha mafanikio na hivyo kuleta matumaini
kuwa huenda gonjwa hilo sugu linalohatarisha maisha ya mamilioni ya watoto
barani Afrika likapatiwa chanjo kwa mara ya kwanza duniani.
Taarifa kuhusu
awamu za mwisho za majaribio ya chanjo hiyo inayotengenezwa na shirika la
GlaxoSmithKline zilitangaza Jumanne ya wiki hii na kuonyesha kwamba ina uwezo
wa kuulinda mwili dhidi ya malaria kwa watoto wenye umri wa miezi mitano hadi
17.
Andrew Witty Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo la kutengeza dawa la Uingereza
ambalo limetengeneza chanjo hiyo amesema kwamba, mafanikio hayo yanaonyesha
kuwa hivi karibuni dunia kwa mara ya kwanza itaweza kupata chanjo ya ugonjwa wa
Malaria.
Hata hivyo sambamba na kusifu mafanikio hayo Bw. Witty amesisitiza
kwamba wanasayansi wanaoshulighulia ugonjwa huo na wataalamu wa masuala ya afya
ulimwenguni kote bado wanasisitiza kwamba chanjo hiyo inayojulikana kana RTS,S
au Mosquirix bado sio njia ya haraka ya kutokomeza malaria.
Licha ya hayo
inaelezwa kuwa chanjo hiyo ya aina ya sindano haina athari sana katika kuzuia
ugonjwa wa malaria ikilinganishwa na chanjo nyingine kama vile za ugonjwa wa
polio na ndui.
Gonjwa la malaria bado ni janga kubwa kwa nchi nyingi duniani hasa za Afrika zilizo chini ya Jangwa la Sahara na kila mwaka hupelekea vifo vya watu wengi kwenye nchi hizo hasa watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano.
Chanjo sio
changamoto pekee inayowakabili wataalamu wa masuala ya afya na tiba duniani
katika kupambana na malaria bali tiba ya ugonjwa huo pia imekuwa ikibadilika
mara kwa mara kutokana na vidudu vya ugonjwa huo kujibadili na kuzishinda nguvu
dawa zinazotengeneza za kutibu ugonjwa huo. Kwa ajili hiyo madaktari na
wataalamu wamekuwa wakishauri kutumiwa zaidi tiba ya dawa mseto katika kutibu
malaria kuliko dawa moja pekee.
Njia nyingine za kujilinda na malaria ni pamoja
na kutumia chandarua, kupiga dawa za kuua mbu na kuyaweka mazingira tuishiyo
katika hali ya usafi bila kuwepo vindimbwi vya maji na kuzungukwa na vichaka
suala ambalo husababisha mbu wazaane.
Ingawa habari hii ni mafanikio makubwa yanayopaswa kupigiwa makofi na wadau wote wa masuala ya afya na tiba lakini, shaka yangu mie ni kuwa, hata kama chanjo hiyo ikianza kufanya kazi kesho lakini je, watoto wote wa bara Afrika wataweza kupatiwa chanjo hiyo na kuepusha na vifo vya holela vinavyosababishwa na malaria? Au isije ikawa hadithi zile zile za chanjo ya polio na ndui ambazo zimekuwepo kwa miongo mingi lakini mpaka leo bado kuna watoto wa Kiafrika wasiopatiwa chanjo hizo kutokana na sababu mbalimbali
Post a Comment