Unachotakiwa kufanya unapokosa hamu ya kujamiiana
Nini unachotakiwa kufanya unapokosa hamu ya kujamiiana
Kwa ufupi
Kukosa hamu ya kujamiiana ni tatizo linalowasumbua wengi nchini. Ni maradhi kwa upande mwingine yanayosababisha ugumba na hata mifarakano na kuvunjika kwa ndoa.
Masanja na mke wake Saumu wameishi kwenye ndoa kwa miaka kumi sasa. Hapo awali, kila kitu kilikuwa sawa katika uhusiano wao, lakini katika miaka ya karibuni, Masanja amekuwa hana matamanio tena na Saumu; hana hamu kabisa ya tendo la ndoa.
Tatizo hili limekuwa likiwaathiri watu wengi hapa nchini na hata duniani kote. Haliwaathiri wanaume pekee kama ilivyo kwa Masanja, bali hata wanawake nao hukumbwa na tatizo hilo.
Utafiti uliofanyika nchini Uingereza , Ulaya na Marekani, ukijumuisha wanawake wa rika zote, ulibaini kuwa asilimia kati ya 30 na 50 ya wanawake wanakumbwa na tatizo la kukosa hamu ya kujamiiana.
Wakati huo utafiti huo ukiweka bayana hilo kutokana na tatizo la uzazi au kukoma kwa hedhi, tafiti nyingne zinaonyesha kuwa karibu robo tatu ya wanawake hawafikii kilele cha tendo hilo au wanapata maumivu.
Wataalamu wa afya wanaeleza kuwa kukosa hamu ya tendo la ndoa kunatibika, iwapo hatua muhimu na za msingi zitachukuliwa.
Ni vyema kufika mapema katika huduma za afya ukiwa na mwenza wako kwa ajili ya uchunguzi na matibabu.
Nini suluhisho la kukosa hamu ya kujamiiana
Kwanza kabisa, inashauriwa kitaalamu kubadilisha mfumo wa maisha kwa mfano, kubadili ratiba za kazi, matembezi au ratiba za wenza.
Kingine ni kufanya mazoezi mara kwa mara kwa sababu mazoezi huongeza ufanisi, lakini pia kupunguza uzito na humfanya mtu kuwa na umbile zuri, furaha na kuongeza ufanisi wakati wa kujamiiana.
Kupunguza msongo wa mawazo kwa kukubali kwamba tatizo lipo baina ya wanandoa na hivyo kutafuta suluhu pamoja na kuacha ugomvi. Matatizo ya kimaisha lazima yatafutiwe ufumbuzi.
Kufanya mazoezi ya misuli ya kiuno kwa kufanya kama unazuia mkojo wakati unahisi haja ndogo na kuhesabu kutoka moja hadi tano, baada ya tano pumzika na halafu rudia. Haya mazoezi (kegel exercise) huongeza uwezo wa kujamiiana kwa wanawake
Kubadilisha mfumo wa maisha kwa wapenzi
Zungumza na mwenza wako – Malumbano na matatizo ni vitu vya kawaida katika uhusiano wowote, ni vizuri kwa wenza kukaa pamoja na kuzungumza matatizo yao, kuwa wa kweli, waaminifu, kuaminiana, kujaliana na kuzungumza juu ya tendo la ndoa kwa pamoja.
Ni vizuri kila mmoja kuainisha vitu anavyopenda na asivyopenda kufanyiwa wakati wa kujamiiana. Pale inapotokea mmoja hajapendezwa au kufurahishwa na uwajibikaji au ufanisi wa mwenzie basi hana budi kutumia lugha nzuri kutafuta kiini cha tatizo na kulitafutia ufumbuzi.
Weka mazingira mazuri na muda wa kufanya tendo la ndoa na mwenza wako ili mpate kudumisha uhusiano wenu.
Ongeza msisimko katika uhusiano wenu kwa kujaribu aina au staili mbalimbali wakati wa kujamiiana, kubadilisha muda wa kufanya mapenzi (sio usiku tu hata asubuhi, mchana) au sehemu tofauti na ile mliyoizoea wakati wa kufanya mapenzi (sio kila siku kitandani).
Kupata ushauri nasaha kutoka kwa wataalamu wa mambo ya uhusiano, ndoa na hata madaktari wa magonjwa ya akili kwani hawa ni weledi zaidi katika kazi yao.
Tiba ya dawa
Kutibu ugonjwa ambao ni kiini cha tatizo hili – Kisukari, magonjwa ya moyo, magonjwa ya zinaa nk.
Daktari kumbadilishia mgonjwa dawa zinazosababisha madhara kama ya msongo wa mawazo na sonona.
Kutibu tatizo la sonona na wasiwasi.
Kutumia dawa au vilainishi vya ukeni wakati wa tendo la ndoa kwa wale wanaopata maumivu au kupunguza uke kuwa mkavu au kuwasha.
Tiba ya vichocheo (homoni)
Dawa za kitaalamu za kuongeza hamu au nguvu atakuandikia daktari baada ya kufahamu kiini cha tatizo. Haishauriwi kutumia bila ushauri wa daktari kwani dawa hizi zina madhara.
Vyakula vinavyosaidia kupunguza tatizo hili
Ikumbukwe ya kwamba vyakula hivi sio tiba mbadala bali husaidia tu kupunguza ukubwa wa tatizo hili la kupungua au kukosa hamu ya kujamiiana na kuboresha kwa wale ambao hawana tatizo hili na hivyo kudumisha uhusiano.
Kitunguu swaumu – Kitunguu swaumu kina kemikali ambayo huongeza mzunguko wa damu kwenda kwenye uume, huongeza hamu ya kufanya mapenzi na utolewaji wa mbegu za kiume.
Habat al soda – Mafuta, mbegu, au unga wa habat soda kama wengi wanavyoiita na ambazo zimetumika kwa miaka mingi sana kupunguza tatizo hili na waandishi wengi wa tiba ya nguvu za kiume wameeleza umuhimu wake. Tumia kidogo kwenye chai au maji ya uvuguvugu mara mbili kila siku. Mbegu hizi hupatikana kwa wingi katika nchi za asia kama Saudi Arabia, Syria, Iran, Dubai (UAE), na hata Misri, Tanzania-maeneo ya pwani hupatikana.
Giligilani – Hii huchochea hamu ya tendo la ndoa kutokana na uwepo kwa wingi wa kichocheo aina ya androsterone.
Ndizi – kuwepo kwa wingi kwa kimeng’enyo aina ya ‘bromelain’ na madini ya potashiam, huongeza msisimko wa tendo kwa wanaume. Potassium pia hupatikana kwenye tikiti maji ambalo pia lina kemikali aina ya ‘arginine’ ambayo huongeza wingi wa damu katika mishipa ya damu na hivyo kusaidia katika kusimika kwa uume.
Parachichi – Huwa na kiwango kikubwa cha madini ya folic acid ambayo huvunjavunja protini. Vitamini B6 kwenye parachichi huchochea kutengeza vichocheo vya kiume kwa wingi.
Mayai – Mayai yana kiwango kikubwa sana cha vitamini aina ya B5 na B6, ambazo husaidia kuleta usawa wa viwango vya vichocheo mwilini na kupunguza msongo wa mawazo.
Nyanya – Zina kiwango kikubwa cha virutubisho aina ya bio-active phyto-nutrients, lycopene, na beta carotene ambazo husaidia kuleta damu kwa wingi kwenye uume na hivyo kusaidia kusimika kwa uume
‘Chocolate’ – Ina kiwango kikubwa cha kemikali ambazo huongeza hamu ya tendo.
Vitamin A – Husaidia katika kuweka usawa wa vichocheo vya mapenzi. Vyakula venye wingi wa vitamin hii ni pamoja na karoti, maini,tikiti maji, spinach, maziwa nk.
Vitamin B complex – Huongeza kiwango cha kichocheo cha testeroneambacho husaidia katika kuongeza ufanisi wa tendo la ndoa kwa wanaume na wanawake. Vitamini B complex hupatikana kwa wingi kwenye ndizi, viazi tamu, lentils mboga za majani, parachichi, mayai, samaki aina ya jodari (tuna), bata mzinga, maini nk.
Mdalasini na Asali– Mchanganyiko wa vitu hivi viwili husaidia sana katika kuongeza ufanisi kwa wale wenye tatizo hili.
Pia
Tendo la ndoa; Tiba mbadala ya maradhi ya moyo, ubongo, maumivu ya kichwa?
>Ingawa tendo la ndoa lisipofanywa kwa kuzingatia kanuni na taratibu, sambamba na umakini, linaweza kusababisha maradhi, lakini kwa wanandoa, tendo hilo linatajwa kuwa na manufaa mengi kiafya tofauti na faraja ya kawaida iliyozoeleka kwa wengi.
Kwa ufupi
- Ikumbukwe kuwa utafiti hauchochei watu kufanya mapenzi kiholela, bali unajikita kwa wanandoa pekee.
Ingawa tendo la ndoa lisipofanywa kwa kuzingatia kanuni na taratibu, sambamba na umakini, linaweza kusababisha maradhi, lakini kwa wanandoa, tendo hilo linatajwa kuwa na manufaa mengi kiafya tofauti na faraja ya kawaida iliyozoeleka kwa wengi.
Imefahamika kuwa tendo hili likifanyika ipasavyo husaidia kuondoa msongo wa mawazo, maradhi ya moyo, maumivu ya kichwa yasiyokoma na kupunguza kasi ya saratani ya tezi dume.
Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Sayansi ya Tiba Muhimbili (Muhas), Dk Yahya Kishashu anasema inategemea tendo linafanywa na nani na mhusika yupo kwenye mazingira gani.
“Kwa mfano, tendo la ndoa linaondoa msongo wa mawazo iwapo unayetenda naye unampenda na amekupa maandalizi mazuri. Sidhani kama alimradi utende hilo tendo na yeyote litakusaidia,” anasema mtaalamu huyo.
Anaongeza kuwa ndiyo maana baadhi ya watu wanatoka nje ya ndoa zao kwa sababu si mara zote tendo la ndoa linawafurahisha wanandoa.
“Wakati mwingine tendo hilo laweza kuwa karaha kwao,” anasema
Mazoezi
Si hivyo tu, utafiti uliofanyika Canada hivi karibuni umebainisha kuwa kufanya tendo la ndoa kwa kipindi cha dakika 25 kwa wanamume kunachoma kalori 100 na kwa wanawake kalori 69.
Tendo hilo likifanyika kwa nusu saa, linaweza kupunguza kalori za mwili kuliko kutembea kwenye mashine ya mazoezi ya ‘treadmill’.
“Ni sawa na kucheza mpira wa tenisi au kutembea ukipanda mlima kwa dakika 20 au kucheza gofu kwa kasi kwa dakika 33 au zoezi la yoga kwa dakika 40,” sehemu ya utafiti hiyo inasema.
Utafiti huo wa Canada ulishabihiana na kampeni iliyofanywa na Taasisi ya Moyo ya Uingereza ambayo ilisema kuwa dakika 30 za tendo la ndoa kwa siku ni muhimu kama mazoezi ya kutembea kwa mashine.
Kwa undani zaidi utafiti huo ulichambua na kusema kuwa, tendo la ndoa, lina manufaa kwa moyo na mapafu.
Inaelezwa kuwa vichocheo vinavyotoka baada ya tendo la ndoa vinasaidia kupunguza kiwango cha msongo wa mawazo na kuongeza uzalishaji wa seli mpya za ubongo.
Kuhusu mazoezi, Dk Kishashu anasema anakubaliana na utafiti huo na kusema kuwa ni kweli tendo hilo linasaidia kupunguza kalori, lakini linapofanyika mara nyingi zaidi linazeesha.
Hata hivyo, wanasayansi wanalipa uzito mdogo tendo hilo katika muktadha wa ujenzi wa hisia na mwili na kuwa halisisitizwi vya kutosha kama aina mojawapo ya mazoezi.
Tiba kwa moyo, mapafu na ubongo
Inaelezwa kuwa tendo la ndoa, linasaidia kuondoa msongo wa mawazo hivyo kupunguza hatari ya maradhi ya moyo.
Si hivyo tu, bali tendo hilo husaidia mapafu kufanya kazi yake vyema, kuingiza na kutoa hewa chafu.
Kitaalamu, upo mchakato uitwao ‘Neurogenesis’ ambao husaidia kulinda seli za ubongo zinazokufa kutokana na uzee. Kuna eneo kwenye ubongo linaloitwa ‘hippocampus’ ambalo ni eneo linalotengeneza kumbukumbu.
“Kazi kubwa inafanyika kwenye ubongo, wakati wa tendo la ndoa, kiasi kikubwa cha viamsha raha huanzia kwenye ubongo na kuleta taarifa kwenye maeneo mengine ya mwili.
Ndiyo maana watu wengi hupotea kiufahamu wakati wa kilele” anasema Dk Gosh, ambaye ni mtafiti.
Hata hivyo, wanaume ambao wanaendelea na tendo la ndoa mara kwa mara hadi wanapofikisha miaka 50 na zaidi, kwa maana ya kutoa mbegu za kiume mara kumi kwa mwezi, wapo katika hatari ndogo ya kupata saratani ya tezi dume. Inaelezwa kuwa mbegu za kiume hazitakiwi kukaa mwilini kwa muda mrefu.Zinatakiwa zitolewe mara kwa mara ili kuzifanya seli mpya zizalishwe. Ni kama kusafisha mpira, inasaidia kusitisha ujenzi wa seli za zamani ambazo zaweza kuwa chanzo cha saratani.
Kwa wanawake, tendo la ndoa husaidia kuundwa kwa misuli ya nyonga ambapo misuli hiyo ikiwa imara huondoa hatari ya kushindwa kuzuia mkojo,(urine incotinence) jambo linaloathiri mwanamke mmoja kati ya wanne wenye umri wa miaka zaidi ya 50.
“ Wakati wa tendo la ndoa, kwa kawaida sakafu ya nyonga za mwanamke hubana na kuachia. Hii husababisha misuli hiyo kuwa imara’ anasema mtafiti huyo.
Hata hivyo, utafiti wa Chuo Kikuu cha Nottingham nchini Uingereza unaeleza kuwa, wanaume wanaofanya tendo hilo na kumwaga mbegu mara 20 hadi 30 kwa mwezi, wapo katika hatari ya kupata saratani ya tezi dume kwa sababu ya umri wao .
Kuondoa maumivu ya kichwa
Utafiti mwingine umebaini kuwa, wanawake wenye umri mdogo hukumbwa na msongo wa mawazo iwapo hawatafanya tendo la ndoa kwa muda mrefu.
Wanawake hao, wanapofika kilele cha tendo hilo, damu hutembea kutoka kwenye ubongo, jambo ambalo huondoa maumivu ya kichwa.
Dk Innocent Mosha, Mchunguzi wa magonjwa wa Hospitali ya Taifa Muhimbili anasema kuwa inawezekana kuwa tendo la ndoa likasaidia kuondoa msongo wa mawazo iwapo mtu hajalifanya kwa muda mrefu na yupo katika hali kubwa ya uhitaji.
“Kama mtu hajafanya tendo hilo muda mrefu na hivyo amelikamia, basi akilifanya litamwondolea msongo wa mawazo,” anasema
Anasema mtu ambaye anahitaji kufanya tendo hilo na hajalipata, aghalabu huwa na msongo wa mawazo lakini kama huliwazi hawezi kuwa na msongo.
Kwenye utafiti huo, wanawake 83 wenye maradhi ya kichwa walipata nafuu kubwa baada ya kumaliza tendo la ndoa.
Ukaribu/ upendo
Mwanasaikolojia, wa Chuo Kikuu cha Dodoma, Modesta Kimonga anasema ni kweli kuwa tendo la ndoa linaleta faraja inayoondoa msongo wa mawazo.
Anasema hali hiyo inatokana na nadharia au mfumo wa uambatano katika saikolojia au ‘attachement theory’
“Hii ‘attachment theory’ ipo kwa watoto wanaponyonya maziwa ya mama zao, na kwa watu wazima ni kwenye tendo la ndoa ambalo linaleta faraja na ukaribu,” anasema.
Anaongeza: “Faraja hupatikana baada ya wanandoa kutenda tendo hilo na huweza kuondoa kabisa mawazo kichwani au huzuni.”
Watafiti walibaini kuwa vichocheo vya ‘oxtocin’ vinavyotolewa wakati wa tendo hilo husaidia hisia za upendo na mshikamano kwenye uhusiano ya muda mrefu.
Lipo ongezeko kubwa la kemikali ya ‘oxtocin’ kwa wanawake na wanaume baada ya kumaliza tendo la ndoa ambalo husaidia kukuza uhusiano na ukaribu wao.
Wanaume kulala baada ya tendo la ndoa
Utafiti wa jarida la Sayansi ya Mishipa ya Fahamu na Tabia uliochapishwa mwaka 2012 umebaini kuwa, dawa za usingizi hufanya kazi sawa na tendo la ndoa kwa wanaume.
Eneo la mbele la ubongo ‘pre –frontal cortex’, ambalo linahusiana na ufahamu, au umakini wa kiakili, huzima au kufungwa baada ya kumaliza tendo hilo.
Kwa baadhi ya utafiti, wanaume kumaliza tendo la ndoa, ni sawa na kunywa dawa za usingizi za ‘diazepam’ zenye ukubwa wa miligramu mbili.
Pia, vichocheo vinavyotoka baada ya tendo hilo kama ‘melatonin,’ ‘oxytocin’ na ‘vasopresin’, zinamsababisha mwanaume apate usingizi mzito.
Post a Comment