Header Ads

MAKADA CCM CHUPUCHUPU KUPIGABA WAKIGOMBEA ENEO

Vurugu hizo ziliibuka jana baada ya baadhi ya makada wa kata ya Moivaro na viongozi wao, kuandamana hadi ofisi za CCM Kata ya Moshono kwa madai eneo hilo ambako kumejengwa ofisi za CCM ni mali yao.

Hali hiyo ilisababisha makada wa pande hizo mbili kurushiana maneno makali karibu kupigana lakini baadhi ya viongozi wa CCM Wilaya waliingilia kati na kuwatuliza.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, baadhi ya makada wa CCM Kata ya Moivaro walisema eneo hilo ni mali yao na kwamba kinachoendelea ni hujuma zinazofanywa na viongozi wa CCM Kata ya Moshono.

Michael Mnyaa na Swalehe Abadalla, kutoka Moivaro walisema wanashangaa uongozi wa CCM Moshono kung’ang’ania eneo hilo kinyume cha sheria ilhali si mali yao.

Wanachama hao walisema suala hilo walishaliwasilisha mbele ya uongozi wa CCM Wilaya na walipewa majibu kwamba ni mali halali ya Moivaro.

Hata hivyo, Rashid Kimario na Eliufoo Mollel, walisema kwa nyakati tofauti kwamba eneo hilo ni mali ya CCM Kata ya Moshono tangu enzi za TANU.

Absolom Loibon, ambaye ni kada wa CCM Kata ya Moshono, alisema chanzo cha mgogoro huo ni kugawanywa kwa kata hizo mbili na kudai kwamba wanaomba serikali irejeshe mipaka ya mtaa wa Kaskazini ili kutuliza hali ya hewa.

Katibu wa CCM Kata ya Moshono, Lucy Siringo, alisema wanashangaa makada wenzao kutoka Moivaro kudai eneo hilo ni mali yao, ilhali wao wamejenga ofisi ya chama.

Siringo alidai kwamba wanahisi kuna njama zinazofanywa na viongozi wa CCM ngazi ya Wilaya kutaka kuwanyang’anya eneo hilo na kutahadharisha kuwa wako tayari kurejesha kadi za CCM endapo mpango huo utafanyika.

Katibu wa CCM Wilaya ya Arusha, Ferooz Bano, alipoulizwa kuhusu suala hilo, alisema wanautambua mgogoro huo na bado unashughulikiwa katika ngazi ya wilaya na kuzitaka pande husika kupunguza jazba.

No comments

Powered by Blogger.