PANYA ROAD WAUNDIWA MIKAKATI KUWAKOMESHA
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, akitoa taarifa ya hali ya usalama wa mkoa huo, mbele ya Rais John Maguli jana jijini Dar es Salaam, alisema kwa muda mfupi kumekuwapo na vikundi hivyo ambavyo vimekuwa vikifanya uhalifu.
Alisema licha ya vikundi hivyo kuanza kutishia usalama, ofisi yake kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama, wameanzisha operesheni maalum ya kuwasaka mitaani wahusika ikiwa hatua ya kudhibiti vitendo hivyo.
“Nikuahidi Rais tutahakikisha kupitia operesheni maalum tuliyoanzisha, tunashughulikia kikamilifu makundi haya ya kihalifu,” alisema Mkonda.
Pia aliwataka wananchi kushiriki kikamilifu kutoa taarifa za kufichua makundi kama hayo ili kuulinda mkoa huo na kusisitiza kuwa kila mwananchi ana jukumu la kulinda usalama wa mkoa kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama.
Mapema wiki hii, Jeshi la Polisi mkoa wa Kipolisi Temeke, liliwatia mbaroni vijana 18 wenye umri kati ya miaka 14 na 20, maarufu kama Panya Road kwa tuhuma za kujihusisha na vitendo vya uhalifu katika maeneo ya wilaya hiyo.
AWACHONGEA WATUMISHI WAVIVU
Mbali na hilo, Makonda aliahidi kumpelekea Rais Magufuli mapendekezo ya watumishi wasio waadilifu ambao wamekuwa wakipokea mishahara ya bure katika mkoa huo bila kufanya kazi.
Alisema bajeti ya mkoa kwa mwaka huu ni Sh. bilioni 662 na kati ya hizo, zaidi ya asilimia 80 zinatumika kulipa mishahara na shughuli za kawaida lakini wanaolipwa mishahara baadhi yao hawafanyi kazi zao.
Alisema kwa mwaka jana zaidi ya Sh. bilioni 81 zilitumika kwa shughuli zingine lakini zaidi ya Sh. bilioni 300 zilitumika kulipia kwenye mishahara kwa watumishi wa mkoa huo.
Makonda alisema watu wanaolipwa mishahara wana elimu za taaluma zao lakini hawataki kufanya kazi na wamekuwa wakilipwa mishahara.
“Mheshimiwa Rais nakamilisha mapendekezo yangu nilete kwako, ikikupendeza mbele za Mungu na mbele za uamuzi wako, nataka ifike hatua tuweke malengo kama watu wa TBA (Wakala wa Majengo Tanzania) walivyoweka malengo ya kufanya kazi kwamba baada ya muda fulani kazi ikamilike.
“Kama mtu hawezi kufanya kazi tumstaafishe kwa manufaa ya umma. Ifike mahali tuwe na watu wanaoweza kufanya kazi na wale wasioweza wakae pembeni, wawe watazamaji,” alisema.
Post a Comment