Namna ya kuishinda Hofu
JINSI YA KUISHINDA HOFU
Mara nyingi inakuwa ngumu kushindana na hofu na wasiwasi unaotokana na mambo mbalimbali ya maisha.
Njia pekee ya kudumu ya kukuwezesha kuzishinda hofu ni kumtegemea MUNGU katika kila jambo. Kila unapokutana na hofu amua kumuangalia MUNGU kwanza na atakuwezesha kuishinda. Zaburi 23:4 Naam, nijapopita katikati ya bonde la uvuli wa mauti, sitaogopa mabaya, kwa maana wewe upo pamoja nami, rungu yako na fimbo yako vyanifariji.
Zaburi 27: 1
BWANA ni nuru yangu na wokovu wangu, nimwogope nani? BWANA ni ngome ya uhai wangu, nimhofu nani?
Anza siku yako kwa maombi. Anza wiki yako kwa maombi na kusoma neno la MUNGU, mweleze MUNGU unavyojisikia na nini hasa hofu yako na umuombe msaada wake wa kukuwezesha kuishinda. Soma mistari inayohusiana na kushinda hofu na uhakikishe unaisimamia.
Jenga tabia ya kumuomba MUNGU uwezo wa kushinda hofu zako kila siku.
Angalia matendo ya MUNGU Hofu inasababisha kutokuona yale ambayo MUNGU anayatenda katika maisha yako.
Usizongwe sana na hofu yako hata ukashindwa kuona jinsi MUNGU anavyokutendea, unapoweka akili yako kwenye ukuu na matendo ya MUNGU taratibu hofu itaondoka ndani yako.
MUNGU hutenda katika hali na wakati usioutarajia, muangalie MUNGU na sio matatizo yanayokuletea hofu.
Kuwa tayari kupokea majibu toka kwa MUNGU.
Mara nyingine hofu husababishwa na kutokuwa tayari kupokea majibu toka kwa MUNGU ambayo yatakuwa kinyume na unavyotaka.
Kumbuka njia za MUNGU si za wanadamu na jawabu la ulimi latoka kwa MUNGU hivyo uwe tayari kupokea majibu toka kwa MUNGU ukijua kuwa yeye anakuwazia yaliyo mema.
MUNGU anajua wewe unahitaji nini hasa katika maisha yako, muamini na uwe tayari kuyafuata mapenzi yake.
JEHOVAH mwenye nguvu akushindie vikwazo vyote na kama hujaokoka kumbuka WOKOVU NI SASA maana hilo ndilo la muhimu kuliko yote ambayo mwanadamu anaweza kuyafanya, Kumpa YESU KRISTO maisha yako ni kupata uzima wa milele maana hakuna uzima wa milele kwingine nje na YESU KRISTO (Yohana 14:6, Matendo 4:12).
Ubarikiwe sana
Post a Comment