Header Ads

Zifahamu hali hatarishi kwa mtu anayetokwa na jasho jingi kupita kiasi,visababishi, na Namna ya kuzuia /kutibu

KUTOKA JASHO JINGI KUPITA KIASI (Exessive sweating) or( Diaphoresis)

Kutoka jasho (sweating) ni jambo la kawaida kiafya kwa binadamu. Kazi mojawapo ya ngozi ni pamoja na kutoa jasho – kitendo ambacho ni muhimu katika kuupooza mwili ili usitunze joto ndani zaidi ya inavyohitajika kiafya. 

Vitengeneza jasho (sweat glands) vipo sehemu zote za mwili, ila mara nyingi zaidi jasho hutoka kwenye kwapa (under arm), kwenye nyayo (feet) au kwenye viganja vya mikono (palms), na hii hutosheleza kuupooza mwili. Kama hii haitoshelezi kupooza mwili basi jasho hutoka popote katika mwili.

Kutoka jasho jingi kwa ghafla (excessive sweating) sio kawaida, huenda ikawa ni dalili ya ugonjwa au tatizo katika mwili linalohitaji uchunguzi zaidi; au hali isiyokuwa ya kawaida katika mwili hata kama sio ugonjwa wenye kuhitaji matibabu.

SABABU ZA KUTOKA JASHO JINGI:

 

SABABU AMBAZO SIO UGONJWA  (Physiological causes)

• Mazoezi makali
• Hali ya hewa ya joto la juu kupita kiasi
• Vyakula vyenye viungo vikali: mfano pilipili kali
• Mabadiliko yatokanayo na kumaliza hedhi kwa wanawake (menopause)
• Kukumbuka jambo lililokuumiza sana (past trauma)
• Hisia kali (kama Hasira, uchungu, woga au wasiwasi)
• Maumivu makali – kama yatokanayo na kuvunjika, kuteguka kiungo kikubwa kama goti au bega
• Madawa ya kulevya – kama cocain, pombe kali; Pia kuacha ghafla au kukosa madawa haya kwa mtumiaji. Mara nyingi hii huambatana na hali ya kutetemeka-tetemeka (tremors) 
• Aina fulani ya dawa za hosipitali – hasa za kutuliza maumivu au zile za matatizo ya kisaikolojia. Kuacha dawa hizi ghafla pia hupelekea kutoka jasho jingi kwa ghafla.
• Sababu za kurithi (genetical factors)

SABABU ZITOKANAZO NA UGONJWA  (Pathological causes)

• Homa kali (fever) – Jasho laweza kutoka kama dalili ya kuwa na homa, au baada ya kutumia dawa za kuondoa homa (kama panado) kama namna ya kuupooza mwili homa inapotoka.
• Vijidudi kwenye damu (infections)– Malaria, virusi (viral illnesses),bacteria n.k
• TB (Tuberculosis) – Jasho jingi hasa wakati mtu amelala, kupungua uzito na dalili nyingine.
• Magonjwa hatari ya moyo (heart attack, heart failure etc) – huenda yakaambatana na kifua kuuma, kukosa hewa, presha kushuka au moyo kwenda mbio.
• Magonjwa hatari ya mapafu – kama damu kuvilia kwenye mapafu (pulmonary embolism), maji kujaa kwenye mapafu(pulmonary oedema), hewa kuzunguka mapafu(pneumothorax)n.k – haya pia huambatana na dalili kama za magonjwa ya moyo zilizotajwa hapo juu.
• Sukari kushuka mwilini (hypoglycemia) – huenda ikaambatana na kuchanganyikiwa, kupoteza fahamu, au kuzimia ghafla. Huwapata sana wagonjwa wa kusukari, hasa wale wanaochoma sindano au kutumia aina fulani ya dawa za sukari.
• Madini joto kuzidi mwilini (hyperthyroidism) – kutoka jasho sana kwenye viganja vya mikono au nyayo wakati wote. Mara nyingi huambatana na dalili nyingine za ugonjwa huu.
• Hali ya presha kushuka sana (Shock) – Hii ni hali ya hatari na huhitaji matibabu ya haraka. Mgonjwa huwa wa baridi, aliyelegea na mwenye kutoka jasho jingi sana mwili wote. 
• Kiarusi (stroke), au magonjwa mengine ya mfumo wa fahamu(nervous system) – haya pia huweza kusababisha jasho kutoka upande mmoja wa mwili hasa magonjwa ya uti wa mgongo
• Saratani za aina fulani – kama saratani ya damu (leukaemia)
• Sumu aina ya mercury na nyinginezo.

Uonapo dalili kama zilizotajwa hapo juu ni muhimu kuwahi hosipitalini, kwani magonjwa mengi yanayosababisha jasho kutoka kwa wingi ni hatari na huweza kusababisha kupoteza maisha. 
 Kama ni mgonjwa wa kisukari anza kwa kumpa kitu chenye sukari kama asali, sukari iliyokorogwa kwenye maji au soda. Kama hana fahamu weka kiasi kidogo chini ya ulimi, kisha mpeleke hosipitali.
 Mruhusu na kumsaidia mgonjwa kukaa kwa namna inayompa nafuu (comfortable position), usimlazimishe kulala au kukaa kwani magonjwa mengine huzidisha ukali/madhara kufuatana na namna ya ukaaji.
 Usimpe mtu anayetoka jasho jingi dawa ya usingizi kabla ya kujua sababu ya jasho kutoka.

JASHO KUTOA HARUFU MBAYA:

Jasho kutoa harufu mbaya sio ugonjwa ila ni hali inayomfanya mhusika kukosa raha na kumpa madhara kisaikolojia. Sababu zifuatazo hupelekea jasho kutoa harufu mbaya:
• Bakteria au fangasi waishio kwenye ngozi (normal skin flora)
• Aina ya vyakula vyenye harufu kali kama vile – vitunguu saumu (garlic)
• Madawa yenye harufu kali
• Magonjwa kama Ugonjwa wa figo ( uremia), Kisukari (DKA)
Kujua sababu inayopelekea harufu mbaya kutakuwezesha kujua njia bora ya kushughilikia tatizo hilo.

MADHARA YATOKANAYO NA KUTOKA JASHO KUPITA KIASI:

• Madini kuvurigika (electrolyte imbalance) – hii hutokana na kupotea kwa madini haya kwa njia ya jasho kama vile madini ya chumvi (Sodium)
• Kupungua maji mwilini (dehydtation) – Hutokea hasa katika mazingira yenye joto kali (kama Dar es salaam), na hii hupelekea mtu kujisikia kuchoka sana, kichwa kizito, kuumwa kichwa na kusikia kikaukiwa sana. Kunywa maji mengi (hasa yenye madini) na maji ya madafu huepusha tatizo hili 
• Madhara ya kisaikologia – mtu anayetoka jasho sana kukosa raha, huweza kujiona sio wa kawaida na pengine kujitenga na wengine(isolation). Hali hii huweza kupelekea msongo wa mawazo (stress or depression)

MATIBABU:

Ni muhimu kutafuta sababu ya kutoka jasho jingi na kutibu chanzo hicho. 
Kwa kuwa magonjwa mengi yanayoambatana na kutoka jasho jingi ni magonjwa ya hatari na yenye kuhitaji matibabu ya haraka, ni muhimu sana kutodharau hali ya kutoka jasho jingi ghafla. Muone daktari kwa ushauri, uchunguzi na inapobidi matibabu.

Kama hakuna magonjwa yanayohitaji matibabu, njia zifuatazo hutumika kutatua tatizo la kutoka jasho kwa wingi:
• Kuoga mara kwa mara – hii husaidia mwili kuwa katika hali ya kupoa hivyo kupunguza jasho, pia husaidia kupunguza vijidudu kwenye ngozi na harufu mbaya.
• Kupumnzika na kuwa katika hali ya utilivu (Relaxation) – Kusinga(massage), mazoezi ya kuvuta hewa nyingi(taking deep breaths) mazoezi ya yoga au kufanya mazoezi ya viungo mara kwa mara husaidia mwili kuwa tulivu (to relax) na hivyo kupunguza au kuondoa hali ya wasiwasi (enxiety) woga (fear) na msongo wa mawazo 
• Dawa za kupaka – Zipo dawa za kupaka ambazo huzuia jasho lisitoke (antiperspirants) , na zipo ambazo husaidia kuondoa harufu mbaya (deodorants).
• Dawa za kumeza, Sindano na Matibabu ya upasuaji – huhitajika tu pale ambapo tatizo ni kubwa na linalomletea mhusika madhara ya kiafya au kisaikologia. Muone daktari wa magonjwa ya ngozi kwa ushauri zaidi.

   Aluminium chloride solution ambayo unaweka kwenye viganja vya mikono na miguu.
   Potassium permanganate.Nimeshawahi kuona botox ikitumika pia lakini ni tiba ya muda hali hio hujirudia.Iontophoresis:
   Njia inayotumia kupitisha maji chini ya ngozi kwa kutumia umeme.
   Upasuaji kwenye nerve ambazo zinahusika na jasho.

1 comment:

Powered by Blogger.