Header Ads

Ufahamu kwa undani ugonjwa wa UKIMWI, nini chanzo,na dalili zake ni zipi?

CHANZO CHA UKIMWI NI NINI?

 

 

Katika mfululizo wa mada hii, nitajaribu kuonyesha ni nini wataalamu mbalimbali wanasema kuhusu ugonjwa wa UKIMWI – tutaona virusi Vya UKIMWI ni nini na nadharia zinazotolewa kuhusu chanzo cha UKIMWI na baadaye kujadili kuhusu dalili za ugonjwa huu, jinsi unavyofanya maambukizi na mwisho jinsi ya kuutibu
ugonjwa wa UKIMWI.

Chanzo cha UKIMWI na VVU ni kitu ambacho kimeendelea kuwaduwaza wanasayansi tangu ugonjwa huo ulipoanza
kujulikana kwenye miaka ya 1980. Kipindi chote toka muda huo, somo hili limekuwa chanzo cha mijadala mikali na nadharia nyingi zimekuwa zikitolewa, kama za mpango wa siri wa chanjo. Ukweli wa suala hili uko wapi? Na ugonjwa huu wa UKIMWI ulitoka wapi haswa?

Ugonjwa huu ulibainika kwa mara ya kwanza kabisa nchini Marekani mwazoni mwa miaka ya 1980. Baadhi ya mashoga (wanaume wanaofanya mapenzi ya jinsia moja) huko New York na california walianza kuonyesha ghafla maambukizi na kansa ambazo hazikukubali tiba ya aina yo yote. Wakati huo, jina la UKIMWI
halikuwepo, lakini ilionekana dhahiri kuwa watu hawa walikuwa wanaugua maradhi yaliyofanana.

Ugunduzi wa Virusi vya UKIMWI ulifuatia mara moja. Ingawa kuna baadhi ya watu wanakataa kabisa hadi leo kuvihusisha virusi hivyo na ugonjwa wa UKIMWI, ushahidi ni wa kutosha kabisa kwamba UKIMWI hutokana na Virusi vya UKIMWI (VVU). Kwa hiyo basi, tukitaka kujua UKIMWI umetoka wapi inatubidi kufahamu kwanza
chanzo cha VVU. Ni vipi, lini na wapi virusi hivi vilianza kuleta ugonjwa kwa binadamu.

 

Virusi Vya UKIMWI  (VVU)

 

Virusi vya UKIMWI ni vya aina ya virusi wanaochukua muda mrefu sana kuleta madhara kwenye mwili baada ya maambukizi (lentivirus), ambao wanashambulia mfumo wa kinga za mwili. Virusi vya aina hii vimeonekana kwenye wanyama wengi wakiwemo paka, kondoo, punda na ng’ombe. Kwa mafaa ya mada yetu ya kutafiti chanzo cha VvU, lentivirus ambaye ni kivitio ni Simian Immunodeficiency Virus (SIV) ambaye hushambulia nyani,
kirusi anayeaminika kuwa na umri wa karibu miaka 32,000.

Inaaminika kuwa VVU ni uzao wa SIV kwa sababu baadhi ya vizazi vya SIV vina tabia za karibu sana na HIV-1 na HIV-2 ambazo ni aina mbili za VVU. HIV-2, kwa mfano, wanafanana sana na S/Vsm ambao ni kizazi cha SIV kilichoonekana kwenye aina ya nyani anayepatikana Afrika Magharibi aitwaye Sooty mangabey au
White-collared monkey. Na aina ya VVU inayosumbua sana na kuambukiza sana, HIV-1 imeonekana kuwa na tabia za S/Vcpz ambaye ni SIV anayepatikana kwa sokwe.

 

white-collared mangabey

 

Mnamo Februari 1999 kikundi cha wanasayansi wa Marekani, baada ya utafiti wa miaka 10 mfululizo kuhusu chanzo cha UKIMWI, walitangaza kuwa waligundua aina ya kirusi wa SIVcpz ambaye alifanana sana na HIV-1. Kirusi huyu aligundulika kutoka aina moja ya sokwe wa Afrika Magharibi na moja kwa moja wakatangaza kuwa
sokwe ndiye chanzo cha kirusi wa UKIMWI cha aina ya HIV-1 na kwamba kirusi huyu aliambukizwa kutoka kwa sokwe hadi kwa binadamu. Wakatoa machapisho kuwa sokwe pori waliambukizwa na aina mbili tofauti za virusi (simian immunodeficiency viruses) kwa wakati mmmoja na katika kujamiiana, alipatikana kirusi wa
aina ya tatu ambaye alienezwa kwa sokwe wengine na hatimaye kwa binadamu na kusababisha UKIMWI.Walieleza pia kuwa makundi yote ya HIV-1 – yaani kundi M, N na O – yaliyotokana na sokwe hawa na kila kundi liliambukizwa kwa binadamu kwa wakati tofauti.
Virusi Vya UKIMWI Vya HIV-1 Na HIV-2.

Virusi vya ukimwi vipo vya aina nyingi sana na vinabadilika haraka sana. Hii ina maana kuwa kuna mikondo mingi ya vizazi vya virusi hata ndani ya mwili mmoja wa mtu aliyeathirika na UKIMWI. Kulingana na tabia za kiurithi, virusi vinaweza kugawanywa kwa aina, makundi na makundi madogo.

Kuna aina mbili za virusi vya UKUMWI: HIV-1 na HIV-2. Aina zote mbili husambazwa kwa ngono, kupitia damu na kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto. Aina hizi mbili huleta madhara yanayofanana lakini HIV-2 haviambukizwi kiurahisi kama HIV-1 na muda kati ya kuambukizwa HIV-2 na kuugua ni mrefu zaidi. Katika dunia watu wengi zaidi huambukizwa HIV-1 na mtu akitamka VVU bila kufafanua, huwa ana maana ya HIV-1. HIV-2 wapo zaidi Afrika Magharibu na hupatikana kwa nadra sehemu nyingine.

Virusi Vya HIV-1

Mikondo ya uzazi wa HIV-1 inaweza kugawanywa katika makundi manne: Kundi kuu M, kundi O na makundi mapya ya N na P. Makundi haya yanaweza kuonyesha namna nne ya jinsi SIV alivyohamia kwa binadamu. Kundi O hupatikana Afrika Magharibu Ya Kati tu na kundi N lililogundulika mwaka 1998 huko Kameruni hupatikana kwa nadra sana. Kundi P lilipatikana kwa mwanamke wa Kameruni mwka 2009. Zaidi ya asilimia 90 ya maabukizi ya HIV-1 ni ya kundi M. Chini ya kundi hili la M, kuna makundi madogo kama tisa yenye utofauti kidogo kitabia, nayo yameitwa A,B,C,D.F,G,H,J,K na CRFs.

 

 

Mara nyingine hutokea virusi vya aina mbili tofauti vikakutana katika seli moja ya mtu aliyeathirika na UKIMWI na kuzaa aina mpya ya kirusi, aina hizi huitwa CRFs “circulating recombinant forms” endapo virusi hivi vipya vitaonekana kwenye miili ya zaidi ya mtu mmoja. CRF A/B ni uzao wa virussi vya makundi madogo
ya A na B.

Aina Za Virusi Na CRFs Hupatikana Wapi?

Makundi haya madogo ya virusi vya UKIMWI vya aina ya HIV-1 na CRFs yamegawanyika kijiografia katika kuonekana kwake na kila eneo fulani la dunia lina kundi fulani lililostawi zaidi ya mengine. Makundi madogo ya HIV-1 yanayoonekana zaidi ni yale ya A na C. Utafiti unaonyesha kuwa sasa watu wanabainika kuwa na aina ya virusi ambavyo si vya asili ya eneo wanaloishi.

. Kundi dogo la A na CRF A/G huonekana zaidi Afrika Ya Kati na Afrika Magharibi. Kundi dogo la A ndilo linalosumbua nchi ya Urusi.

. Kundi dogo la B lina historia ya kupatikana bara la Ulaya, Marekani, Japan na Australia. Hili ni kundi linalopatikana hasa kwa wanaume wanaoshiriki ngono ya jinsia moja (mashoga).

. HIV-1 ya kundi dogo la C imeenea zaidi sehemu za Afrika Ya Kusini na Afrika Mashariki, India na Nepal. Hili ndilo kundi lililoleta madhara zaidi ya makundi mengine yote na nusu ya watu wote ambao wana UKIMWI wameathiriwa na kundi hili la kirusi.

 

 

. Kundi la D hupatikana Afrika ya Kusini na Afrika Mashariki tu. CRF A/E kupatikana zaidi kusini mashariki mwa Asia lakini lilitokea Afrika ya Kati. Kundi dogo F limeonekana Afrika Ya Kati, Marekani Ya Kusini na Ulaya Ya Mashariki. Kundi G na CRF A/G yameonekana Afrika Magharibi na Afrika Mashariki na Ulaya Ya Kati.

. Kundi dogo H limeonekana Afrika Ya Kati, kundi dogo J Marekani ya Kati na K hupatikana Kongo (DRC) na Kameruni tu.
Mategemeo ni kuwa makundi madogo ya UKIMWI na CRFs yatazidi kupatikana kutokana na kuwa makundi huzaliwa pale kirusi wa kundi moja anapokutana na kirusi wa kundi jingine na makundi haya yaliyopo yatazidi kuenea na kuonekana maeneo mengine ambako sasa hivi hayajaonekana.

 

Kuna Uhusiano Wa Aina Ya Kirusi Na Kupata UKIMWI?

Utafiti mmoja uliofanyika nchini Uganda mnamo 2006 ulionyesha kuwa watu walioambulizwa virusi vya UKIMWI vya kundi dogo D au/na CRFs zake walipata UKIMWI mapema zaidi kuliko wale wa kundi dogo A na walikufa mapema zaidi kama hawakupewa tiba ya ARV. Watafiti hao wakashuri kuwa kundi dogo hili la D ni hatari
zaidi kwa kuwa linajishika zaidi kwenye seli za kinga za mwili. Ufafiti unaofanana na huo ulifanyika pia nchini Kenya mwaka 2007 kwa wanawake wenye virusi hao wa kundi dogo D na kuonyesha kuwa walikuwa kwenye hatari ya kufa zaidi ya wale waliokuwa na kundi dogo A. Utafiti mwingine nchini nchini Senegali (1999) ulionyesha kuwa wanawake wengi zaidi walioathirika na makundi madogo C, D na G walipata UKIMWI katika miaka miatano baada ya maambukizi mapema zaidi kuliko wale wa kundi dogo A.

Utafiti mwingine nchini Thailand ulionyesha kuwa watu wailokuwa na virusi vya kundi dogo CRF A/F walipata UKIMWI na kufa mapema zaidi kuliko wale wa Kundi dogo B,  kama hawakupata tiba ya ARV.

No comments

Powered by Blogger.