Header Ads

Fahamu namna saratani inavyo tokea na namna ya kujikinga na kutibu

UGONJWA WA KANSA NI NINI? CHANZO NA AINA ZA SARATANI.

 


Kama umekuwa ukisikia kuhusu ugonjwa wa kansa au saratani na ukawa unajiuliza ni nini ugonjwa huu wa kansa, pitia ukurasa huu ambamo tutatazama maana ya ugonjwa huu, chanzo chake, madhara anayoweza kupata mtu mwenye ugonjwa huu na tiba ambazo hutolewa kukabiliana na tatizo la kuumwa na ugonjwa huu wa kansa.

Kansa (saratani) ni neno lililotolewa kwa kundi la magonjwa yanayosabahiana. Kuna aina tofauti zaidi ya 100 ya magonjwa yanayoitwa kansa au saratani. Katika aina zote hizi za saratani, baadhi ya seli za mwili huanza kujigawa bila kusimama na kuenea kwenye maeneo ya karibu ya mwili. Kansa huweza kuanza kwenye
sehemu yo yote ya mwili. Kwa kawaida seli za mwili hujigawa na kuzalisha seli mpya kulingana na mahitaji ya mwili, seli za zamani zikiharibika au kuzeeka, seli mpya huchukua nafasi ya seli hizo.

Saratani inapotokea, mpangilio huu huvurugika. Kadri uvurugikaji huu unavyozidi, seli za zamani zinaendelea kuishi badala ya kufa na seli mpya hutengenezwa bila mahitaji ya mwili. Seli hizi za ziada
huendelea kujigawa na kujenga uvimbe (tumors). Saratani za aina nyingi hujenga uvimbe isipokuwa saratani za damu, kama leukemia, ambapo ugonjwa huu huzuia ufanyakazi kazi wa kawaida wa damu kwa kusababisha kugawanyika kwa seli za damu kusiko kwa kawaida.

Uvimbe unaotokana na saratani ni hatari kwa maisha, huweza kuenea kwenye maeneo ya karibu ya mwili na kadiri unavyokua baadhi ya seli huweza kujitoa kutoka eneo moja zikasafiri kupitia mfumo wa damu hadi eneo jingine la mwili na kuanza kujenga uvimbe mpya kwenye eneo hilo jipya mbali kabisa na eneo la
awali. Uvimbe wa saratani huweza ukakua na kuvuruga utendaji kazi wa mfumo wa mmeng’enyo wa chakula, ubongo na mfumo wa damu. Uvimbe unaotokana na saratani ukiondolewa, huweza kurudia kujijenga upya kabisa.

 

Chanzo Cha Kansa

 

Kansa ni ugonjwa unaotokea katika viini vya mwili vinavyohusika na kurithisha tabia kutoka kizazi kimoja hadi kingine (genes) – ni ugonjwa unaotokana kwa kubadilika kwa genes zinazohusika na ufanyaji kazi wa seli za mwili, na hasa zile zinazohusika na namna seli zinavyokua na kujigawa.

Mabadiliko katika genes yanaweza kuwa ya kurithi kutoka kwa wazazi au yanaweza kutokea katika kipindi cha maisha ya mtu kutokana na hitilafu zilizotokea wakati wa kugawanyika kwa seli au kutokana na uharibifu wa DNA uliotokana na vitu vilivyopo kwenye mazingira viitwavyo carcinogens. Vitu vya kwenye mazingira vinavyosaidia kuharibu DNA na kukua kwa kansa (carcinogens) ni kama kemikali zilizopo ndani ya moshi wa tumbaku, asbestos, arsenic, mionzi ya gamma, X-rays, moshi wa magari na mionzi ya jua  (UV rays).

Umri wa mtu unapokuwa  mkubwa uwezekano wa kutokea dosari katika mabadiliko ya DNA yanayosababisha kansa huongezeka na kufanya umri kuwa ni sababu moja ya kuweza kupata kansa kirahisi. Kuna virusi wanaohusishwa na kansa kama human papillomavirus (wanaosababisha kansa ya cervics ), hepatitis B na C (wanaosababisha kansa ya ini), Epstein-Barr virus (anayesababisha baadhi ya kansa za utotoni), Human immunodeficiency virus (HIV) -na kitu cho chote kinachodhoofisha kinga za mwili.

Kila mtu mwenye saratani ana mmchanganyiko tofauti wa sababu zilizopelekea kutokea mabadiliko hayo katika genes zake. Kansa inavyozidi kukua, mabadiliko za ziada huongezeka. Uvimbe mmoja unaweza kuwa na seli zilizozalishwa kutokana na aina tofauti ya badiliko katika genes.

Kansa iliyoenea kutoka sehemu moja ya mwili ilipoanzia hadi sehemu nyingine huitwa metastatic cancer na tendo la kansa kuenea kutoka sehemu moja hadi sehemu nyingine ya mwili huitwa metastasis. Kansa iliyoenea kutoka sehemu moja ya mwili hadi sehemu nyingine huwa na aina ya seli zilezile za sehemu ambako ilitokea na hupewa jina lile lile la aina ya kansa ya sehemu ya mwanzo ilikotokea. Kwa mfano, kansa ya ziwa iliyoenea na kwenda kujenga uvimbe katika mapafu haitaitwa kansa ya mapafu bali metastatic cancer ya ziwa na uchunguzi kwa vyombo maalumu wa seli za sehemu hizi mbili utaonyesha kufanana kwa seli za sehemu hizo mbili toauti. Kansa hizi zinazotokea kwa kuenea kutoka sehemu moja ya mwili hadi nyingine (metastatic cancers) huleta madhara makubwa kwa ufanyaji kazi wa mwili na idadi kubwa ya watu
wanaofariki kwa saratani, hufariki kwa sababu ya aina hii ya kansa.

Aina Za Kansa

 

Mara nyingi aina za kansa hutajwa kutokana na kiungo ambako kansa hiyo ilianzia. Kwa mfano, kansa iliyoanzia kwenye mapafu itaitwa kansa ya mapafu na ile iliyoanzaia kwenye ubongo itaitwa kansa ya ubongo. Kuna namna nyingine za kuzitofautisha kansa, kama vile kwa kutaja aina ya seli zilizozijenga kansa hizo.

Hapa chini ni baadhi ya makundi ya kansa zilizoanzia kwenye aina fulani ya seli:

Carcinoma
Carcinomas ndizo kansa zinazoshambulia zaidi watu kuliko aina nyingine zote za kansa. Kansa hizi zinajengwa na seli zinazofunika maeneo ya ndani na ya nje ya mwili (epithelial cells) ambazo zipo za
aina nyingi.

 

 

Carcinoma hupewa majina kutokana na aina ya seli zilipoanzia:

Adenocarcinoma ni kansa zinajojenga seli za epithelial zinazozalisha majimaji au ute. Kansa nyingi za maziwa, utumbo na tezi kuu huwa ni za aina hii (adenocarcinomas).

Basal cell carcinoma ni aina ya kansa inayoanzia kwenye tabaka la chini la epidermis – epidermis ni sehemu ya juu ya ngozi ya mwili.

Squamous cell carcinoma ni kansa inayojenga kwenye seli ziitwazo squamous cells – ambazo ni seli za epithelial zilizo chini ya ngozi mara baada ya sehemu ya juu kabisa ya ngozi. seli za Squamous pia hufunika viungo vingine vingi vya mwili ikiwa ni pamoja na tumbo, utumbo, mapafu, kibofu cha mkojo na figo. Kansa za aina hii pia huitwa epidermoid carcinomas.

Pia kuna aina ya kansa iitwayo Transitional cell carcinoma ambayo hushambulia ngozi inayofunika kibofu cha mkojo, ureters, sehemu za figo na maeneo mengine.

Sarcoma
Kundi hili la kansa linajumuisha saratani zinazojenga kwenye mifupa na sehemu laini za amwili kama kwenye misuli, mafuta, mishipa ya damu. mishipa ya lymph, tendons na ligaments.

Katika kansa za mifupa osteosarcoma ndiyo inayoshambulia idadi kubwa zaidi ya watu. Osteosarcoma huanzia kwenye seli za kuzalisha mifupa mipya (osteoblasts) na ni aina saratani amabya hushambulia zaidi vijana wa umri mdogo. Saratani hii mara nyngi hujenga sehemu inapoishia mifupa mirefu ya mwili ambayo ni mifupa ya mikono na miguu. Kwa watoto wachanga na wale wa umri wa zaidi ya miaka kumi, hujenga zaidi karibu na magoti.

Dalili kuu za osteosarcoma ni uvimbe kwenye eneo la mfupa, maumivu kwenye mfupa au joint na kuvunjika kwa mfupa kusikoambatana na sababu yo yote ile. Kansa hii huchochewa na tiba ya mionzi na matumizi ya vidonge vya kuzuia kansa vinavyoitwa alkylating agents.

Aina nyingine ya kansa ya mifupa inaitwa Ewing sarcoma.

Aina za kansa zinazoshambulia viungo laini vya mwili ni leiomyosarcoma, Kaposi’s sarcoma, malignant fibrous histiocytoma, liposarcoma na dermatofibrosarcoma protuberans.

 

 

 

 

Kaposi sarcoma au kaposi’s sarcoma ni aina ya kansa inayojenga au kuleta mabadiliko kwenye viungo vya ngozi, utando laini wa kwenye midomo, pua na koo na maeneo mengine ya mwili.

Leukemia
Hizi ni kansa zinazoanzia kwenye sehemu za uzalishaji wa chembechembe za damu zilizopo ndani ya mifupa
(bone marrow). Kansa hizi hazijengi uvimbe wa namna yo yote bali huongeza idadi kubwa ya chembechembe nyeupe za damu zilizo za kipekee katika damu na katika eneo la uzalishaji wa chembechembe za damu (bone marrow) na kuzizidi kabisa chembechembe nyekundu za damu kiidadi. Hali hii ikitokea mwili hushindwa
kupata kiwango cha hewa ya oksijeni kinachotakiwa ili viungo vyake vifanya kazi vizuri, hushindwa kudhibiti utokwaji wa damu mwilini na kupambana na maambukizi.

Leukemia ni kansa inayowapata zaidi watu wenye umri wa zaidi ya miaka 55 na watoto wadogo chini ya miaka 15 na mara nyingi hutibiwa kwa chemotherapy.

 
Lymphoma
Lymphoma ni kansa inayoanzia kwenye Tcells au B cells au kwa neno jingine lymphocytes ambazo ni seli nyeupe za kupambana na magonjwa – ni sehemu ya kinga za mwili. Saratani hii inapotokea, seli hizi zisizo za kawaida hujijenga kwenye mishipa ya lymph na sehemu nyingine za mwili.

Kuna aina kuu mbili za lymphoma:
Hodgkin lymphoma – hizi huanzia kwenye B cells
Non-Hodgkin lymphoma – Hiki ni kikundi kikubwa cha kansa zinazoanzia kwenye lymphoctes. Kansa hizi hukua haraka sana au taratibu na zaweza kuanzia kwenye B cells au T cells.

 
Multiple Myeloma
Hii ni aina ya kansa inayoanzia kwenye seli za plasma, ambayo ni aina nyingine ya seli zinazohusika na kinga ya mwili. Seli hizi za kansa zisizo za kawaida (myeloma cells) hujengwa kwenye sehemu ya mifupa inayohusika na ujenzi wa seli za damu (bone marrow) na husababisha uvimbe kwenye mifupa yote ya mwili. Kansa ya aina hii pia huitwa plasma cell myeloma au ugonjwa wa Kahler.

 
Melanoma
Melanona ni aina ya kansa inayoanzia kwenye seli zinazojenga melanin – vitu vinavyoipa ngozi ya mwili rangi yake. Melanomas nyingi hujenga juu ya ngozi ya mwili lakini mara nyingine huweza kujenga kwenye sehemu tofauti ya mwili yenye rangi, kama kwenye macho.


Dalili Za Kansa

 

Ugonjwa wa kansa una ishara nyingi ambazo hutegemea zaidi kansa hiyo ipo kwenye sehemu gani ya mwili, imekwisha enea kwa dalil za melanomakiwango gani na ukubwa wa uvimbe wa kansa hiyo. Kansa nyingine huonekana kwa macho au kwa kupapasa juu ya ngozi – uvimbe juu ya ziwa au kwenye korodani huweza kuwa ishara ya kansa. Kansa aina ya melanoma mara nyingi hutambuliwa kutokana na mabadiliko ya vijipele juu ya ngozi. Kansa nyingine hutoa mabaka meupe ndani ya midomo au madoa meupe kwenye ulimi.

Kansa nyingine hutoa dalili ambazo hazionekani dhahiri. Uvimbe wa kwenye ubongo, mathalani, huathiri jinsi mtu anavyoweza kutambua vitu na kansa za kwenye kongosho hazitoi ishara mapema hadi maumivu yatakapoanza pale neva za maeneo ya karibu zitakapoanza kuminywa au shughuli za ini zitakapoathiriwa na kusababisha ngozi na macho kuwa ya rangi ya njano (jaundice).

Ishara nyingine zitaonekana uvimbe utakapoanza kusukuma viungo vya karibu au mishipa ya damu. Kwa mfano, kansa za kwenye utumbo huweza kusababisha kukosa choo kikawaida, kuharisha au kiasi cha kinyesi kinachotolewa. Kansa za tezi dume huathiri ufanyakazi wa kibofu cha mkojo na kusababisha kupata haja ndogo mara kwa mara au kutopata haja ndogo.

 

ishara za kansa

 

Kwa vile seli za kansa hunyonya nguvu za mwili na kuvuruga mfumo wa kinga za mwili, ishara nyingine za homa, uchovu, kutokwa jasho, kukosa damu, kupungua uzito kusiko na sababu huweza kutokea.

Kansa iliyoenea hadi kwenye maeneo ya ubongo husababisha kizunguzungu na maumivu ya kichwa. Kansa ya mapafu inawezaa kusababisha kukohoa na kupumua kwa shida. Ini linaweza kuwa kubwa na kusababisha ugonjwa wa homa ya manjano, mifupa huweza kuuma na kuvunjika kirahisi.

Tiba Ya Kansa

 

Tiba ya ugonjwa huu wa saratani inatolewa kwa kutegemea aina ya kansa aliyo nayo mgonjwa, kansa hiyo imeenea kiasi gani katika mwili wa mgonjwa huyo, umri wa mgonjwa, afya aliyo nayo na mambo mengine yanayoendana na mgonjwa huyo. Hakuna tiba ya wote na mara nyingine mgonjwa atapewa mchanganyiko wa tiba
na uangalizi. Tiba zilizopo zinaangukia katika makundi yafuatayo: upasuaji, mionzi, chemotherapy, immunotherapy, hormone therapy au gene therapy. Tutapitia kwa kifupi aina hizi za tiba za kansa hapa
chini.

Tiba Ya Kansa Kwa Upasuaji: Tiba ya kansa kwa upasuaji ndiyo tiba ambayo imetumika kwa muda mrefu zaidi kuliko tiba nyingine zote. Endapo kansa ya eneo moja haijaenea kwenye sehemu nyingine ya mwili, mgonjwa anaweza kupona kabisa kwa tiba hii ya uapasuaji. Mafanikio makubwa kabisa ya tiba hii yameonekana katika tiba za kansa za maziwa na kansa za tezi dume. Kansa ikiishaenea toka sehemu moja ya mwili hadi nyingine, tiba hii haiwezi kuondoa seli zote za kansa.

Tiba hii inapotumika kwa sasa hivi kuondoa uvimbe, madaktari huondoa kipande cha seli za kawaida kuzunguka eneo la seli za kansa kuhakikisha kuwa seli zote za kansa zimeondolewa. Mgonjwa hulazilka kubaki kwenye nusu-kaputi wakati vipimo vinachukuliwa kuhakikisha kuwa eneo la kiada lililoondolewa halina seli za kansa na kwa bahati mbaya wakigundua uwepo wa seli hizo za kansa, humrudia mgonjwa na kukata kipande zaidi.

Maendeleo ya teknolojia sasa hivi yamekuja na kifaa kipya kitwacho IKnife ambacho chenyewe hugundua seli za kansa hivyo kuwawezesha madaktari kujua upeo wa eneo la kulikata na kuondoa seli zote za kansa bila ya kusubiri vipimo vya kwenye maabara.

 
Tiba Ya Kansa Kwa Mionzi: Tiba hii ambayo pia huitwa radiotherapy huondoa kansa kwa kuelekeza mionzi yenye nguvu kwenye seli za kansa. Mionzi hii huziharibu seli hizo na kuzifanya zijiue zenyewe. Tiba hii ya mionzi hutumia mionzi yenye nguvu inayoitwa gamma-rays inayotolewa na machine maalumu.

tiba ya mionzi ya saratani

Tiba za mwanzo kwa kutumia mionzi zilikuwa na madhara makubwa ya kuharibu seli za kawaida lakini maendeleo katika teknolojia yameiboresha tiba hii na sasa mionzi hiyo ina uwezo wa kulenga seli za kansa kwa uhakika zaidi na hivyo kutoleta madhara kwa seli za kawaida. Radiotherapy hutumika kufanya uvimbe unywee au kuharibu seli za kansa (pamoja na kansa za aina ya leukemia na lyphoma). Tiba hii hutumika pia pamoja na tiba nyingine za kansa.

Tiba Ya Kansa Ya Chemotherapy:Chemotherapy ni tiba inayotumia kemikali ambazo zinavuruga tendo la seli za mwili kujigawa na kusababisha seli hizo kujiua zenyewe. Tiba hii hulenga zile seli ambazo zinajigawa kwa haraka na kwa kawaida hutumika kutibu kansa zilizoenea kutoka eneo moja ya mwili hadi eneo jingine
(metastatic cancers) kwa sababu kemikali hizi zina uwezo wa kusambaa katika mwili wote wa mgonjwa. Hii ni tiba ya lazima kwa aina fulani ya kansa za aina ya leukemia na lymphoma.

tiba ya chemotherapy

Chemotherapy hutolewa kwa vipindi ili mwili uweze kupona katikati ya dozi moja na nyingine. Madhara ya tiba hii ni pamoja na
kunyonyoka nywele, kichefuchefu, uchovu wa mwili na kutapika. Ni tiba ambayo mara nyingine hutolewa kwenda sambamba na tiba nyingine za saratani.

Tiba Ya Kansa Ya Immunotherapy: Immunotherapy ni tiba inayokusudia kuziongeza kinga za mwili ili mwili uweze kupambana na uvimbe. Sindano inaweza kudungwa kwenye eneo lililoathirika ili uvimbe unywee (Local immunotherapy). Namna nyingine ni kuuwezesha mwili wote kuongeza kinga ili kupambana na uvimbe katika sehemu zote za mwili (Systemic immunotherapy). Tiba hii bado ni changa lakini zimeonyesha mafanikio katika kutibu kansa za maziwa.

Utafiti unaendelea na kila siku wanasayansi wanakuja na tiba nyigine na kuzijaribu. Tiba ambazo zipo kwenye majaribio ni pamoja na Gene therapy yenye lengo la kukarabati genes zilizoharibika.kwa


Ahsante

No comments

Powered by Blogger.