DEREVA WA BODABODA AGONGA FUSO NA KUFA
FRANK
Ndunguru (24), mkazi wa Mbinga mjini, amekufa papo hapo baada ya bodaboda
aliyokuwa akiendesha kugonga gari aina ya Mitsubishi Fuso kwa nyuma.
Ndunguru alikutwa na mauti alipokuwa akiendesha chombo hicho akitokea Mbinga mjini kwenda Mbamba Bay wilayani nyasa.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, Zuberi Mwombeji, alisema jana ofisini kwake kuwa tukio hilo lilitokea juzi saa tatu asubuhi, katika eneo la Tangi la Maji, Mbinga mjini, baada ya bodaboda hiyo yenye namba za usajili MC 238 AUJ, aina ya SunLG kugonga Fuso iliyokuwa imebeba mizigo.
Alisema Ndunguru aligonga gari hilo kwa nyuma lililokuwa likiendeshwa na Said Mohamed (36) kutoka Mbinga kwenda Mbamba Bay, likiwa limesheheni mizigo.
Mwombeji alisema chanzo cha ajali hiyo ni mwendokasi wa dereva wa bodaboda aliyekuwa akiendesha bila kuchukua tahadhari, hali ambayo ilimfanya ashindwe kuumudu usukani.
Alisema kuwa chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi wa mwendesha bodaboda hivyo, amewataka waendesha bodaboda kuwa makini wanapoendesha bodaboda hizo.
Wakati huo huo, Mwombeji alisema polisi mkoni humo, katika wilaya ya Tunduru, juzi walikamata watu wanne wakiwa na lita 13.5 za pombe haramu aina ya gongo ikiwa kwenye ndoo tayari kwa kuuza.
Aliwataja watu waliokamatwa katika doria iliyofanyika katika kata ya Kichangani kuwa ni Hadija Hamanzi (24), Abdalah Hashim (20), Rashidi Charles (42) na Shabani Mussa (29), wote wakazi wa Kijiji cha Kadewele, Tunduru.
Pia alisema katika wilaya ya Songea, polisi wakiwa kwenye doria eneo la Bombambili, walimkamata Mapambano Seif (30) akiwa na gramu 250 za bangi alizokuwa amehifadhi kwenye mfuko wa plastiki.
Kamanda Mwombeji alieleza kuwa watuhumiwa wote katika matukio mawili tofauti, wanatarajiwa kufikishwa mahakamani baada ya upelelezi kukamilika.
Post a Comment