Header Ads

Supastaa sehemu ya 3

Simulizi za Nyemo
NYEMO CHILONGANI
SUPASTAA-03
ILIPOISHIA..
SOFIA: Alikukumbatia kwa furaha?
PHIZA: Hapana.
SOFIA: Sasa kilitokea nini?
PHIZA: Ngumi. Ugomvi ambao hakukuwa na mtu
aliyeweza kuuzima.
ENDELEA NAYO
PHIZA: Kwanza yule jamaa alikuwa akiniangalia
kwa macho ya chuki, alionekana kunikumbuka
kwamba mimi ndiye nilikuwa yule msela wa kipindi
kile nilichomfuata Stellah nje ya gari huku nikiwa
muhuni, nilimuita lakini aliamua kuondoka.
Kwa jinsi jamaa alivyokuwa akinicheki, ilionekana
wazi kwamba ni lazima ningepokea kichapo mahali
hapo. Alipoona Stellah amenifuata na
kunikumbatia, alisaga meno yake kwa hasira.
Hakuendelea kuwa kwenye hali hiyo, alishindwa
kabisa kuvumilia, akanifuata na kuanza kunipiga
mikwara.
SOFIA: Ikawaje hapo kwa mtoto wa Tandale
kupigwa mikwara.
PHIZA: Unajua nilibadilika. Kipindi cha nyuma
nilikuwa mhuni sana lakini katika kipindi hicho
nilibadilika. Nilijua fika kwamba endapo
ningeanzisha mtiti wangu jamaa angeshindwa
kabisa kuuzima na sidhani kama kungekuwa na
mtu ambaye angeuzima, nikajifanya kutulia tu.
Jamaa alinisukumasukuma huku na kule na hata
kunikunja shati langu. Akaichomoa tai yangu na
hata ule usmart wa kuchomekea ukatoka. Jamaa
wa duka lile alikuwa pembeni, kwanza yeye
mwenyewe alishangaa ni kwa sababu gani mshikaji
alikuwa akinifanyia vile, eti kisa demu jamaa
alikuwa akinizingua kihivyo.
Jamaa alipoona nimekuwa mpole huku Stellah
akimuomba anikaushie, mshikaji akazidi kujiona
yeye tembo, akaendelea kunikunjakunja kiasi
kwamba kikafika kipindi nikaanza kummaindi.
SOFIA: Ikawaje?
PHIZA: Nikaona kama ningeendelea kujifanya
mnyonge mshikaji angenipanda kichwani, na mimi
nikaanza kumletea timbwili. Ilikuwa ni kizaazaa
mtu wangu. Jamaa alikuwa akinikunjakunja tu
lakini mi sikufanya hivyo, kitu cha kwanza
nikampiga apakati.
SOFIA: Apakati ndiyo nini?
PHIZA: Hiyo ni aina ya ngumi unayopigwa ubavuni.
Nilipompiga apakati ya kulia na kumalizia ya
kushoto, mshikaji akakaa chini na kuanza kuugulia
maumivu.
Wanawake waliokuwa mahali hapo ambao walikuja
kununua mashela walikuwa wakishadadia kwamba
nilichokifanya kilikuwa sahihi kabisa kwani jamaa
ndiye alikuwa chanzo.
Unajua mapenzi mapenzi tu. Huwezi amini Stellah
alikuwa upande wangu. Aliishia kububujikwa na
machozi huku akinikumbatia. Kuna kitu nilianza
kukiamini, unajua unaweza kuwa na mtu ambaye
unahisi kwamba unampenda lakini ukweli wa moyo
wako ni kwamba mapenzi ya dhati yapo kwa mtu
mwingine kabisa.
Hivyo ndivyo ilivyokuwa kwa Stellah, ni sawa
alikuwa na msela lakini kwangu alionekana kuwa
tofauti sana, alionekana kunipenda mno mpaka
nikashangaa.
SOFIA: Ikawaje baada ya mshikaji kuugulia
maumivu.
PHIZA: Unafikiri msela alirudia, ngumi nzito
nilizompa zikamfumbua macho kwamba sikuwa
mtu wa mchezo hata mara moja, hata
aliposimama, hakutaka kubaki hapo, akatoka zake,
akaingia ndani ya gari na kusepa.
SOFIA: Kwa hiyo hakuondoka na Stellah?
PHIZA: Hakuondoka naye, alimuacha, nikawa sina
jinsi, nikajichukulia mtoto kiulainiiii, kama nanawa
vile.
SOFIA: Hahaha! Na vipi siku hiyo, jamaa mwenye
duka alikusaidia?
PHIZA: Hakuna. Nilikwishakinukisha hapo na
kumfukuzia mteja wake, unafikiri angenisikiliza
tena! Alinimaindi kinoma, akanitimua, nikaondoka
na Stellah wangu.
SOFIA: Mlikwenda wapi?
PHIZA: Stellah alinichukua na kuelekea kwenye
mghahawa fulani hivi upo hapo Afrika-Sana,
tukakaa na kuanza kula. Aliniuliza maswali mengi
mno, nilimsimulia mpaka kipindi kile nilichomfuata
huku nikiwa msela, alishangaa sana, hakuamini
kama nilikuwa mimi.
Ndiyo hivyo, tuliendelea kupiga stori na aliniuliza
nilifuata nini kwenye duka lile, nikamwambia
kwamba nilihitaji fedha na jamaa alikuwa ameahidi
kunisaidia ila baada ya ugomvi, msela akanitosa.
Alichokifanya, akanitaka tuondoke mahali hapo.
Tukaelekea mpaka pale Kijiweni, akateremka
kutoka kwenye bajaji na kuelekea katika mashine
ya ATM, akatoa kiasi cha shilingi milioni moja,
akanikabidhi.
SOFIA: Mmmh! Ulijisikiaje?
PHIZA: Siwezi kuielezea furaha niliyoisikia kipindi
hicho. Nakiri kwamba Stellah amenifanikisha kufikia
mahali hapa, kwani kiasi kile cha fedha
nilichokipata nikakitumia katika kurekodi wimbo
wangu wa kwanza unaoitwa Malaika, nafikiri
unaukumbuka.
SOFIA: Naukumbuka sana. Si ndiyo uliokutoa!
PHIZA: Yeah!
SOFIA: Ulijisikiaje kuingia studio kwa mara ya
kwanza?
PHIZA: Acha aiseee....nilijisikia furaha isiyo
kawaida. Nakumbuka siku hiyo nilikwenda na
Stellah mpaka studio, ilikuwa ni furaha kubwa, kila
nilipokuwa nikiiangalia studio ile nilijisemea
kwamba huo ndiyo utakuwa mwanzo wa ndoto
zangu za kuwa mwanamuziki mkubwa hapo
baadae.
Hata nilipoanza kuimba, nilijisikia kufarijika. Katika
kila mistari niliyoiimba ndani ya chumba kile,
nilikuwa nikimwangalia Stellah tu, bado alikuwa
msichana mrembo sana ambaye sidhani kama
niliwahi kukutana naye kabla.
Nilitumia zaidi ya masaa kumi studio, baadae
nikaondoka, ilikuwa kama saa kumi na mbili jioni
hivi. Kuna kipindi nilikuwa nikimwangalia Stellah,
sikufichi, kama mtu unampenda, anapokuwa na
kitu moyoni ambacho hakimpi furaha, utagundua
tu. Ndivyo ilivyokuwa kwa Stellah.
SOFIA: Ulimuuliza?
PHIZA: Ndiyo. Nilitaka kujua tatizo nini.
SOFIA: Akasemaje?
PHIZA: Alikuwa na kitu ambacho hakutaka
kuniambia. Alitakiwa kusafiri kuelekea nchini
Marekani, alikuwa amebakisha siku tatu tu za
kuishi nchini Tanzania. Unajua ngoja nikwambie
kitu Sofia. Nilihitaji kuwa karibu na Stellah kwa
kipindi kirefu sana, nilikuwa nimekwishamzoea.
Tulipomaliza darasa la saba, nilikuwa nimempoteza
hivyo sikutaka kumpoteza tena, nilitaka niendelee
kuwa naye siku zote za maisha yangu.
Ila ikawa haina jinsi, siku ilipofika, akasepa zake na
kuelekea Marekani kusoma, aliniambia kwamba
angechukua miaka minne ya masomo.
SOFIA: Maisha yalikuwaje bila Stellah?
PHIZA: Yalikuwa ni magumu, muziki bila msichana
ilikuwa ni mateso. Japokuwa niliishia darasa la
saba lakini nakumbuka kuna mstari kwenye wimbo
fulani wa Timberland aliomshirikisha Drake uitwao
Say Something ambapo kuna mstari Drake alisema
‘What's a star when its most important fan is
missing?’ yaani akimaanisha kuna umuhimu gani
wa kuwa staa na wakati shabiki muhimu
amekosekana?
Hivyo ndivyo ilivyokuwa kwangu, yaani hata Stellah
alipoondoka na kuelekea Marekani, nilikuwa
mnyonge, wakati mwingine nilikuwa nikibaki
chumbani na kuanza kujiuliza kwa nini aliondoka
katika kipindi muhimu kama hicho.
SOFIA: Kuna changamoto gani ulizipata?
PHIZA: Hapo ndipo kulipokuwa na kazi Sofia.
Nilikuwa nimetoa Wimbo wa Malaika lakini
kuwafanya watu wausikilize ilikuwa shughuli sana.
Katika redio nyingi nilipokuwa nikiwapelekea
wimbo wangu kwa ajili ya kuupiga walinitaka
nilipie kiasi fulani cha fedha, hakika kwangu ilikuwa
ngumu sana kwa kuwa sikuwa na fedha.
Nilipata tabu sana mpaka kufikia kipindi nilipokuwa
nikiona kuna kijisherehe uswahilini Tandale,
nilikuwa nikienda na kuwaomba niimbe, tena bure
kabisa, walikuwa wakinikubalia ila mwisho
waliamua kunipoza elfu kumi.
Hayo ndiyo yalikuwa maisha yangu. Wimbo wangu
ulikubalika sana lakini haukuwa ukisikika redioni
hivyo hakukuwa na raia wengi waliokuwa
wakiusikia.
SOFIA: Ila ndiyo wimbo ambao ulikutoa na kupigwa
sana redioni kuliko nyimbo za wasanii wote,
ilikuwajekuwaje hapa?
PHIZA: Elimu ni kitu bora sana. Unajua hata ukiwa
tajiri bila kuwa na elimu, kuna vitu unakosa. Kuna
siku nilikuwa nimechili tu kwenye Camp yetu ya
watoto wastaarabu ya Mafyoso Camp, kuna msela
alikuja, alikuwa na demu wake fulani hivi, demu
fulani mkali sana...hahaha! Ila hajamshinda
Stellah.
Alipokuwa akipita, akaniona, akanifuata na kuanza
kunipa darasa la ujasiriamali. Sikuwa nikimfahamu
na sidhani kama alikuwa akinifahamu lakini
aling’ang’ania sana kunipa darasa hilo. Kiukweli
nilimuona msela akinizingua sana, alipomaliza
somo lake huku nikiwa sijaingiza kitu chochote kile
zaidi ya kuona akinipigia kelele, akaniuliza kama
nilikuwa na biashara, nikamwambia sina.
Jamaa akasikitika weee, mwisho wa siku akasema
nilikuwa na kipi cha kufanya, nikamwambia muziki
ila wimbo wangu wangu haukuwa ukipigwa
redioni. Msela akanipa idea fulani ambayo sikuwa
nimeifikiria kabisa, akanitaka niuchukue wimbo
wangu na kuwapelekea watu wa bodaboda na
bajaji wawe wanaupiga kila siku.
SOFIA: Duuh! Kumbe umepitia mbali,
PHIZA: Wee acha tu. Nikaanza kuusambaza wimbo
huo, ilikuwa kazi lakini namshukuru Mungu kwani
masela waliupokea na kuanza kuupiga.
Niliusambaza sehemu mbalimbali ikiwepo Tandale,
Mwananyamala, Kijitonyama, Manzese na sehemu
zote, huko kote wana wakawa wanaupiga.
Huwezi amini Sofia, baada ya mwezi mmoja tu
wimbo wangu kupigwa na waendesha bodaboda na
bajaji, nilipigiwa simu kutoka kituo fulani cha redio
kwa ajili ya interview, nikaenda na hapo ndipo
nilipoanza kuupata usupastaa.
Baada ya hiyo interview na wimbo kupigwa,
nikaanza kupata matamasha, nikapiga sana
matamasha ila dau langu lilikuwa ni shilingi laki
moja, ikizidi sana laki mbili. Nilipiga sana na
kufanikiwa kung’aa.
Sikuamini siku moja nasikiliza redio fulani,
nikashtuka kusikia wimbo wangu umeshika namba
moja, nilibaki nikibubujikwa na machozi ya furaha
chumbani. Nilirukaruka sana.
SOFIA: Huo ndiyo ukawa mwanzo wa mafanikio
bila shaka. Na vipi kuhusu chuchuziii, hawakuanza
kusumbua?
PHIZA: Hahaha! Aiseee! Chuchuziii tena!
Utawaeleza nini hapo. Demu wa kwanza kabisa
kuwa naye toka nilipoanza kuukwaa ustaa alikuwa
huyu My X, Bertha ambaye juzijuzi tu
nilimkosakosa kumpiga na risasi kwa kuwa
aliwazingua wazazi wangu.
SOFIA: Ulikutana naye wapi?
PHIZA: Hahaha! Daaah! Bertha...Bertha
...Bertha...nilikutana naye kwa mara ya kwanza
pale Maisha Klabu.
SOFIA: Ikawaje.
PHIZA: Daah! Ni stori ndefu sana. Yaani kwa
matukio yote ambayo Bertha amenifanyia mimi na
wazazi wangu, acha tu afanye vile, alistahili.
Mapenzi niliyompa, nahisi hakuwahi kuyapata kwa
mtu yeyote yule, hata huyo jamaa aliyekuwa naye
sijui kama aliwahi kumpa mapenzi kama
niliyompa.
SOFIA: Yapi hayo?
PHIZA: (Ananyamaza na kuanza kucheka)
Je, nini kiliendelea?........

No comments

Powered by Blogger.