Header Ads

Supastaa sehemu ya 2

Simulizi za Nyemo
NYEMO CHILONGANI
SUPASTAA-02
ILIPOISHIA
SOFIA: Kwa hiyo hukuwahi kumwambia ukweli?
PHIZA: Hahaha! Mbona unakuwa na presha Sofia?
Subiri.
SOFIA: Sawa, nakuwa mpole, tiririka mwanaume.
PHIZA: Daah! Stellah!
ENDELEA NAYO
PHIZA: Huu uzuri alionao Stellah, ulikuwa
hivyohivyo toka kipindi cha nyuma. Unajua Sofia
umasikini ni mbaya sana, unapokuwa nayo,
automatic moyo wako unakosa kujiamini,
unapowaona wanawake wazuri, moyo wako
unakwambia kwamba huyo si msichana
anayetakiwa kuwa nawe kwa kuwa huna kitu,
ndivyo ilivyotokea kwangu na Stellah.
Nilijua fika kwamba Stellah alikuwa akinipenda,
lakini ningefanya nini masikini mimi, nikaamua
kubaki kimya tu. Kila siku Stellah alikuwa akiniita
na kunitaka nimwangalie katika kipindi alichokuwa
akifanya mazoezi ya kuwa mwanamitindo.
SOFIA: Ilichukua muda gani mpaka kumwambia
ukweli?
PHIZA: Kipindi kirefu, tulizoeana sana na tulipofika
darasa la saba, hapo ndipo nilipoamua kumwambia
ukweli. Siku hiyo nilijiandaa vilivyo, nilifua nguo
zangu vilivyo, nilikuwa nimenyoa na kesho yake
safari ya shuleni ilianza.
Stellah aliutesa sana moyo wangu. Najua kwa sasa
ananisikiliza kwa kuwa nilimpigia simu na
kumuuliza kama ingekuwa sahihi mimi
kulizungumzia suala hilo kwenye televisheni na
alinikubalia. Stellah, wewe ni msichana wa tofauti
sana kwangu, nilikupenda sana na siwezi kujizuia,
bado moyo wangu unakupenda mno.
SOFIA: Ikawaje baada ya kujiandaa sana kwa
kunyuka pamba zilizopigwa pasi?
PHIZA: Hahaha! Acha tu. Nilipofika shule, hakuwa
amefika hivyo nikamsubiria huku moyo wangu
ukiwa na presha kubwa. Siku hiyo, mara kwa mara
nilikuwa nikijitazama kama nilikuwa nimependeza
au la.
Japokuwa nilikuwa masikini sana lakini kwa siku
hiyo nilikuwa tofauti sana. Baada ya dakika kadhaa,
Stellah akafika shuleni hapo. Sikufichi, siku hiyo
alionekana kuwa tofauti kabisa na siku nyingine,
alikuwa mrembo hasa, aliponiona tu, akaanza
kunisogelea huku akiachia tabasamu pana.
Akanisalimia, muda wote mapigo yangu ya moyo
yalikuwa yakidunda sana kana kwamba moyo
ulitaka kuchomoka.
SOFIA: Hahaha! Hukumkumbatia?
PHEZA: Weeee! Ningeanzaje? Mwili ulikuwa
ukinitetemeka mno. Kuna kipindi aligundua hilo na
kila alipotaka kuuliza, nilikuwa nikimpa maongezi
mengi mfululizo ili mradi tu asiongee kitu chochote
kile.
Baada ya mapumziko, nikaomba kuonana naye in
private, akanikubaliana na hivyo kukaa naye
sehemu moja.
SOFIA: Ulimwambia?
PHIZA: Nilimwambia.
SOFIA: Akasemaje?
PHIZA: Alishtuka sana, akaniangalia mara
mbilimbili, akajifanya kutokuamini kile
nilichomwambia. Yaani ishara zangu zote
nilizokuwa zimemuonyeshea, leo hii alikuwa
akijifanya kushangaa.
SOFIA: Akasemaje? Yes au No?
PHIZA: Daaa! Huwezi kuamini, Stellah alikasirika
sana. Kuanzia siku hiyo, akakata mawasiliano nami
tena alinitishia kwamba angekwenda kumwambia
mwalimu wetu wa darasa. Kiukweli nilinyong’onyea
sana.
Kuanzia siku hiyo, nikajiona kuwa kama panya na
Stellah kuwa paka. Kila nilipomuona, nilijificha na
nilipokuwa nikimuona akiongea na marafiki zake,
hata kama walikuwa wakipiga stori nyingine nilihisi
kama wananizungumzia mimi.
SOFIA: Hahaha! Ikawaje sasa mtu mzima? Manake
sikupatii picha kipindi hicho, ukawa mdogo kama
priton vile.
PHIZA: We acha tu, yaani tena bora ya priton,
nilijiona mdogo kama mchanga wa baharini.
SOFIA: Kwa hiyo huo ndiyo ukawa mwisho?
PHIZA: Kitu kilichokuwa kikinishangaza ni kimoja
tu. Stellah alikuwa amenikasirikia sana lakini
alikuwa akiongoza kwa kuniangalia darasani.
Unajua kwa sisi vijana wa zamani hasa miaka ya
90 ukiona msichana anakuangalia sana, unahisi
kwamba anakupenda, tofauti na mwaka huu wa
2016.
Nakumbuka siku ya mwisho kabla ya kufanya
mtihani wa taifa wa darasa la saba, Sofia
akaniandikia Wimbo wa Nitamwambia ulioimbwa na
The Ruler, nadhani unamkumbuka.
SOFIA: Yeah!
PHIZA: Alijua kwamba niliupenda sana wimbo huo
na ndiyo maana mashairi yote alikuwa
ameniandikia huku akisisitiza kwamba alikuwa
akinipenda ila hali ya kunikataa ilikuwa imetokea
tu.
Sikufichi Sofia, nilifurahi mno, nilishindwa kujizuia,
usiku wa siku hiyo nikaondoka nyumbani kuelekea
kwao Tabata kwa miguu. Nilipofika huko, nikaenda
kwenye kibanda cha simu na kuomba kupiga simu,
nikampigia na kutoka nje.
SOFIA: Hahaha! Kweli ulipenda. Kutoka Tandale
mpaka Tabata kwa miguu tena usiku?
PHIZA: Ndiyo hivyo. Nilipofika nikaonana naye na
kupiga naye stori. Kwa mara ya kwanza siku hiyo
ndiyo nikabadilishana mate na msichana, japokuwa
kipindi cha nyuma niliwaona watu wanaofanya
hivyo kwamba ni wachafu, lakini kwangu nilijisikia
poa kabisa.
SOFIA: Na hali ya nyumbani ilikuwaje kipindi
hicho?
PHIZA: Unafikiri basi kulikuwa na mabadiliko,
hakuna, bado maisha yalikuwa yaleyale tu. Baada
ya hapo tukafanya mitihani, Stellah akafaulu na
mimi kufeli. Yeye akajiunga na Jangwani
Sekondari, ile shule ya Wasichana na mimi kuingia
maisha ya mitaani.
Hapo ndipo nilipoanza kufikiria kwamba nilitakiwa
kufanya kitu kingine cha ziada. Hapo nilikuwa na
miaka kumi na tano. Nikaanza ishu ya kuuza ice
cream nyumbani kwa mzee mmoja ambaye ni
marehemu, huyo mzee Madevu aliyewasaidia
wazazi wangu fedha za hospitalini.
Nilifanya biashara ile kwa kipindi cha mwaka
mzima, biashara ilikuwa ngumu sana. Kuna wakati
mwingine nilikuwa nikikutana na majanga kama
kupigwa na kunyang’anywa deli la ice cream,
wakati mwingine matusi kutoka kwa wanafunzi
kwamba sikutakiwa kufanya biashara ile.
Nilipofikisha miaka kumi na sita, mwaka 1999 ,
nikaanza kujichanganya na makundi ya mitaani.
Hayakuwa makundi makundi mazuri. Nakumbuka
kipindi hicho kwa Tandale, kulikuwa na camp moja
tu ambayo ilikuwa nzuri na ambayo vijana wake
hawakuwa wahuni, hii iliitwa Mafyoso Camp, ila
hizo nyingine ikiwepo ile ambayo nilijiunga nayo
iitwayo Mazaga, ilikuwa ni ya kihuni sana.
Unavyoniona hapa, nimekwishawahi kuvuta sigara,
bangi, nilishawahi kubwia unga na uchafu
mwingine mwingi tu, hata kubaka nilikwishawahi
kubaka ila namshukuru Mungu sikuathirika.
SOFIA: Pole sana. Ikawaje baadae? Haukumtafuta
Stellah?
PHIZA: Kwanza nashukuru Mungu katika kipindi
hicho sikuonana na Stellah kwani angenishangaa
sana kwani nilikuwa mhuni mkubwa tu.
Mwaka 2003 ambapo The Ruler anatoa Wimbo wa
Nitakutafuta Tu, ndipo nikakumbuka kwamba
kulikuwa na mtu ambaye nilitakiwa kumtafuta,
huyu alikuwa Stellah. Sikujua ningempata wapi
kwani hata nilipojaribu kwenda kwao, mlinzi wa
getini hakutaka kuniruhusu kuingia kwani aliniona
mhuni sana, akanifukuza.
SOFIA: Pole sana, ikawaje baada ya hapo.
PHIZA: Nakumbuka baada ya kufukuzwa na mlinzi,
nikaondoka zangu huku nikiwa nimejiinamia.
Nilipofika pale Mwananchi, nikamuona msichana
ambaye hakuwa mgeni machoni mwangu, alikuwa
amesimama nje ya gari fulani hivi akiwa na
mwanaume, nilipomwangalia vizuri, nikagundua
kwamba alikuwa Stellah, alipendeza mno.
Huku nikiwa na kipensi changu, kaoshi kwa juu na
huku nikitembea kwa kudunda, nikamsogelea
Stellah, aliponiona, hakunijua, nilikuwa tofauti sana,
sura yangu ilikuwa imekwishaharibiwa mno.
Nilipomfikia, nikamuita. Akashtuka, akaniangalia
kwa makini huku akivuta kumbukumbu kwamba
alikwishawahi kuniona sehemu lakini bahati mbaya
hakukumbuka. Nilipoendelea kumsogelea, yule
jamaa aliyekuwa naye ambaye alionekana kuwa
smart sana akanizuia, hakutaka niendelee
kumsogelea.
Nilijaribu kumuita tena Stellah lakini hakuonekana
kujali kwa kuwa hakunitambua.
SOFIA: Kwa hiyo hata hukujitambulisha?
PHIZAL Huo ndiyo ujinga nilioufanya.
Niling’ang’ania kumuita lakini sikujitambulisha,
akaingia ndani ya gari na kuondoka zao.
SOFIA: Ulijisikiaje moyoni?
PHIZA: Kuna maumivu ambayo unaweza
kuyaelezea lakini kuna mengi ambayo kamwe
huwezi kuyaelezea. Ni afadhali angekuja mtu
mmoja na kunichanachana na wembe ningesikia
nafuu lakini si vile ambavyo Stellah alikuwa
amenifanyia. Niliumia mno.
Hebu jifikirie, kwa ajili ya mapenzi, nilitoka Tandale
mpaka Tabata tena kwa mguu, n imefika kule,
nikafukuzwa na mlinzi, niliporudi, nakutana na mtu
niliyemfauata halafu haonekani kunijali,
ungejisikiaje? Hivyo ndivyo nilivyojisikia.
SOFIA: Ikawaje hapo baadae?
PHIZA: Nilirudi nyumbani huku nikiwa na majonzi,
nilichokuwa nimekigundua ni kwamba vilevi ndivyo
vilivyokuwa vimeniharibu, hivyo nilitakiwa
kuachana navyo. Kitu cha kwanza nilichokifanya ni
kuachana na camp mbaya na kuhamia Mafyoso
Camp. Haikuwa kazi rahisi, kwa kuwa hawakuwa
wahuni, nilipowasogelea, walinitenga sana ila
baadae wakanizoea na kuanza kuwa nao,
nikaachana na madawa na hivyo kuwa kijana
mzuri.
Mwaka mmoja baadae, nikagundua kwamba
nilikuwa na kipaji cha kuimba hivyo nilitakiwa
kuwa msanii kama wengine. Nilichoshauriwa ni
kumtafuta The Ruler. Kiukweli nilipafahamu
alipokuwa akiishi zamani kabla hajawa staa, hivyo
nilitakiwa kumfuata.
Hiyo ilikuwa mwaka 2004, nikafanikiwa kwenda
alipokuwa akiishi, ilikuwa maeneo ya Sinza Mori,
nilipofika kule, sikuweza kumpata. Mwaka mzima
nikawa namtafuta yeye lakini bado sikufanikiwa
kumpata kwa ajili ya kumshirikisha wimbo wangu.
SOFIA: Vipi kuhusu Stellah?
PHIZA: Kiukweli sikupata mawasiliano naye tena,
niliamua kuwa kivyanguvyangu tu. Nilihangaika
sana kutunga nyimbo nzuri lakini sikupata fedha za
kurekodia, hivyo niliendelea kusota mtaani huku
nikiishi maisha ya kugongea, leo nakula hapa,
kesho nakula kule.
Ilipofika mwaka 2006, huwezi amini, nilikakutana
na Stellah kwa mara nyingine tena, mara hii
ilikuwa ni katika duka moja hivi kule Sinza, lilikuwa
duka la kukodisha mashela ya harusi. Nilikwenda
hapo kwa kuwa mmiliki aliniambia kwamba niende
ili anisaidie japo kiasi fulani cha fedha kwa ajili ya
kurekodi nyimbo zangu.
SOFIA: Ulipomuona Stellah ilikuwaje? Alikuwa peke
yake?
PHIZA: Kwanza nilifurahi sana, aliponiangalia usoni,
akaonekana kunikumbuka. Sikuwa mhuni kama
kipindi kile, nilikuwa mtanashati japokuwa sikuwa
nimevaa nguo za gharama. Hakuwa peke yake,
alikuwa na yule jamaa niliyemkuta naye siku ile,
yule mchizi smart.
SOFIA: Nini kilitokea?
PHIZA: Hahahaha! Otea!
SOFIA: Alikukumbatia kwa furaha?
PHIZA: Hapana.
SOFIA: Sasa kilitokea nini?
PHIZA: Ngumi. Ugomvi ambao hakukuwa na mtu
aliyeweza kuuzima.
Je, nini kitaendelea?.......

No comments

Powered by Blogger.