Header Ads

Supastaa sehemu ya 1

Simulizi za Nyemo
NYEMO CHILONGANI
SUPASTAA
Jina lake lake aliitwa Phillip Zachariah ila
alijulikana zaidi kama Phiza. Huyu alikuwa
mwanamuziki mkubwa aliyekuwa akitamba nchini
Tanzania. Umaarufu wake ulimpatia fedha nyingi,
akatembea na wanawake wengi huku akibadilisha
magari kadri alivyotaka.
Kipindi cha nyuma, hakuwa tajiri kama watu
walivyokuwa wakidhani, na yeye alikuwa masikini
mkubwa ambaye alipigana kila siku mpaka kuwa
na fedha kama alizokuwa nazo sasa.
Katika maisha yake, kulikuwa na watu wengi
ambao walikuwa wakila kupitia yeye, walikuwa
wakibadilisha nguo na magari kupitia yeye. Phiza
hakuwa mchoyo, kila alipofuatwa na mtu mwenye
shida, alimsaidia pasipo kuangalia alikuwa nani.
Watanzania wengi wakatamani kuyajua maisha
yake, wengi wakapiga simu katika Kituo cha
Televisheni cha Global ili mtangazaji mahiri, Sofia
Michael afanye mahojiano na mwanamuziki huyo
na Watanzania wenye kiu ya kutaka kufahamu
alipotoka mwanamuziki huyo wapate kufahamu.
Kumpata Phiza halikuwa jambo jepesi hata kidogo,
kila siku alikuwa akipigiwa simu, jibu lake lilikuwa
moja kwamba hakuwa jijini Dar es Salaam. Kama
ulikuwa haujamzoea, ungeweza kusema kwamba
alikuwa akiringa lakini kile alichokuwa
akikizungumza ndicho kilikuwa ukweli wenyewe.
Hakuwa mtu wa kutulia, leo alikwenda Shinyanga,
kesho alikwenda Kigoma na mtondogoo alikwenda
Kilimanjaro, maisha ya kuzunguka huku na kule
ndiyo yalikuwa maisha aliyokuwa akiishi.
Baada ya miezi minne kupita, mtangazaji Sofia
akafanikiwa kumpata Phiza, aliamua kwenda
kumpokea mwenyewe uwanja wa ndege alipokuwa
akitoka Marekani, huko, akamuomba sana aonane
naye kesho katika jumba kubwa la kituo cha
Televisheni cha Global, Phiza akakubali.
Siku iliyofuata, gari lenye thamani ya shilingi
milioni 200 lilikuwa likipaki katika eneo la jengo
hilo na kisha mwanamuziki mwenye sura nzuri
kuteremka na kuanza kupiga hatua kuelekea ndani
ya jengo hilo.
Baadhi ya watu waliokuwa mahali hapo, wakaanza
kumpiga picha kwa simu yao huku wengine
wakiomba kupiga naye picha, bila kinyongo na bila
maringo, akakubali kupiga nao picha.
SOFIA: Umependeza sana
PHIZA: Asante, hata wewe umependeza pia.
Niambie, what’s next.
SOFIA: Twende ndani.
Wakaanza kuondoka nje ya jengo hilo na kuingia
ndani. Ilikuwa studio nzuri lakini kwa Phiza
ambaye alikuwa ametembelea studio nyingi Afrika
Kusini, Malawi na nchi nyingine, ile ilionekana
kuwa ya kawaida.
SOFIA: Ninataka kuanza kipindi, upo tayari?
PHIZA: Kama kawa. Vipi kuhusu mapoda?
SOFIA: Usijali, kuna dada atakufanyia yote hayo.
Wala haukupita muda mwingi, dada mmoja,
mrembo mwenye asili ya kiarabu akamfuata na
kuanza kumfanyia ‘make up’ kabla ya kuanza
kipindi, alipomaliza, akaruhusiwa na kukaa sehemu
husika, kamera zilikuwa mbele ila hazikuwa
zimewashwa.
SOFIA: Upo tayari?
PHIZA: Yaap yaap....kwa hiyo nizungumzie nini
sasa?
SOFIA: Historia ya maisha yako, ila utakuwa ukijibu
maswali yangu.
PHIZA: Hakuna noma.
SOFIA: Twende hewani.
Hapohapo kamera zikawashwa. Watanzania wengi
walikuwa mbele ya televisheni zao, kila mmoja
alikuwa na shauku ya kutaka kufahamu historia ya
maisha ya Phiza, kule alipotoka mpaka kuingia
katika ulimwengu wa kuogelea fedha.
Maisha yake yalikuwa siri lakini siku hiyo, mbele
ya kamera, alikuwa tayari kuzungumzia kila kitu
kilichotokea katika maisha yake, likiwepo suala la
kuupata umaarufu kupitia muziki wake.
SOFIA: Karibuni sana watazamaji wetu wa Kipindi
cha Keeping Up With Sofia ambacho kinaletwa na
Kituo chako Bora cha Global. Leo, kama ilivyo
kawaida yetu tunakuletea msanii anayetamba sana
kwa sasa nchini Tanzania, huyu si mwingine bali ni
Phillip Zachariah au kwa jina jingine la a.k.a
hujulikana kama Phiza.
PHIZA: (Anatoa tabasamu pana)
SOFIA: Karibu sana Phiza.
PHIZA: Asante sana.
SOPHIA: Kwanza ningependa ujitambulishe kwa
watazamaji kabla haujaanza kusimulia kile
kilichotokea katika maisha yako.
Phiza akaanza kujitambulisha kwa ujumla,
japokuwa watu wengi walikuwa wakimfahamu lakini
kwake haikuwa tatizo, alipomaliza, akamgeukia
Sofia.
SOFIA: Asante. Sasa uwanja wako.
PHIZA: Koh koh koh (alianza kwa kukohoa)
Ukiniangalia kwa sasa hivi na kisha mtu akatokea
na kukwambia kwamba nilikuwa masikini kama
asilimia kubwa ya Watanzania walivyo, nahisi
utakataa. Kitakachokufanya kukataa ni kwa sababu
unaiona gari yangu aina ya Range SV ya milioni
200, unaziona nyumba zangu za kifahari, unaiona
ndege yangu na kusikia kiasi cha fedha
nilichokuwa nacho benki.
Sofia, nilikuwa masikini kama wengine, sikuzaliwa
na fedha na hata wazazi wangu hawakuwa na
fedha. Nilimsikia mara kwa mara mama akiniambia
kwamba siku ambayo alinizaa hospitalini,
hawakuwa na fedha, gharama zote ambazo
walitakiwa kulipia hospitalini, zililipwa na majirani
zangu, mzee Mkude, bi Amina na mzee mmoja
ambaye kwa sasa ni marehemu, mzee Issa
Madevu.
SOFIA: Kwa hiyo ulizaliwa katika familia masikini
sana?
PHIZA: Naweza kusema hivyo. Mara baada ya
kuzaliwa, mama alikaa hospitalini kwa siku mbili
na ndipo akaruhusiwa kutoka na kurudi nyumbani.
Kipindi hicho walikuwa wakiishi Tandale na
nilizaliwa katika Hospitali ya Mwananyamala.
Of course kulikuwa na daladala, lakini hawakuwa
hata na senti tano, huku mama akiwa mgonjwa-
mgonjwa, wakaanza kutembea kwa miguu kurudi
nyumbani huku baba akiwa amenibeba
(ananyamaza, anafumba macho na kuyafumbua
tena, machozi yanaanza kujikusanya machoni
mwake, anaendelea...)
Mama alizidi kuniambia kwamba nyumbani
hakukuwa na kitu, siku hiyo ambayo walirudi
nyumbani, hakukuwa na chakula, walikaa tu ndani
huku nikilia mno, nilionekana kuwa msumbufu
lakini ndiyo tayari nishakuwa mtoto wao,
wangefanya nini sasa? Wakaamua kunionyeshea
mapenzi ya dhati.
Baada ya kukaa kwa takribani masaa mawili,
majirani wale waliokuwa wamejichangisha fedha
kulipia gharama wakafika nyumbani hapo na
kuwapa hongera wazazi wangu na kisha kuwaachia
kiasi cha fedha kwa ajili ya matumizi.
SOFIA: Ikawaje?
PHIZA: Siku hizo zilikuwa ni za mateso makubwa,
nilikuwa msumbufu sana kwa kulia, mama alikuwa
akininyonyesha japokuwa kuna siku alikuwa
zilikuwa zikipita bila kula kitu chochote kile.
Baada ya miezi sita, baba akaanzisha biashara ya
kuuza samaki. Alikuwa akiwatoa samaki kule Feri
na kuwaleta Tandale ambapo alikuwa akiwauza.
Kidogo akaanza kupata fedha za kubadilishia
chakula.
SOFIA: Kwa hiyo kipindi hicho mlikuwa kwenye
nyumba ya kupanga?
PHIZA: Ndiyo. Familia yetu ilikuwa masikini sana.
Unajua unaweza kusema masikini halafu mtu
mwingine akachukulia poa, ninaposema masikini,
elewa kwamba ni masikini kupitiliza.
Kabiashara hako kakaendelea. Ndiyo iliyokuwa
ikiingiza fedha kwa ajili ya matumizi ya nyumbani.
Kuna watoto wa majirani walikuwa wakivalishwa
pempas lakini amini usiamini, sikuwa kuvalishwa
vazi hilo, kitu pekee nilichokuwa nikivalishwa ni
kanga na nailoni, nilipokuwa najisaidia, mama
aliitoa kanga ile ambayo ilikuwa kama tambala na
kisha kuifua, ilipokauka, akanivalisha tena, hayo
ndiyo yalikuwa maisha yetu.
SOFIA: Biashara ya baba yako iliendeleaje?
PHIZA: (Haongei kitu kwanza, ananyamaza kwa
muda na kumwangalia Sofia, anayafumba tena
macho yake na kuyafumbua, machozi yanaanza
kumbubujika) Baba alifilisika. Sijui ilikuwaje. Mama
aliniambia kwamba alifilisika kwa kuwa fedha
zilitumika zaidi kwangu kuliko kuziendesha
biashara tuliyokuwa nayo.
SOFIA: Ikawaje baada ya hapo?
PHIZA: Baba akaanza kukaa nyumbani.
Alichokifanya ni kujifundisha ujenzi. Alikuwa na
rafiki yake mmoja, jina lake silikumbuki na ndiye
alikuwa mtu pekee ambaye alimsaidia baba katika
kumtafutia kazi ya ujenzi sehemu mbalimbali.
Bado maisha yalikuwa ni ya shida mno, umasikini
ulitutafuna sana. Leo unaponiona naendesha gari la
kifahari, wazazi wangu wanakula maisha, acha tu
wale. Maisha tuliyopitia ni ya dhiki mno,
ninawapenda sana wazazi wangu na ndiyo maana
my Ex Bertha aliponitukania wazazi wangu miezi
kadhaa iliyopita nikataka kumpiga risasi.
Walinihangaikia mpaka kufika hapa, leo sitaki
waguswe wala kudharauliwa.
SOFIA: Ikawaje baada ya hapo?
PHIZA: Baba aliendelea na kazi ya ujenzi kwa
miaka kadhaa. Baada ya miaka saba, nikaanza
darasa la kwanza, hiyo ilikuwa mwaka 1994.
SOFIA: Kwa hiyo hukusoma chekechea?
PHIZA: Sikusoma kwa sababu bado gharama
ilikuwa kubwa, walichoona kufaa ni kunipeleka
darasa la kwanza. Kiukweli sikuwahi kushika nafasi
za juu, naweza kusema kwamba sikuwa na akili
darasani. Kila mtihani nilitoka wa mwisho, kidogo
nilipoingia darasa la nne, nikafanikiwa kufaulu
mtihani wa taifa na kuingia darasa la tano.
SOFIA: Maisha ya nyumbani yalikuwaje wakati
huo?
PHIZA: Umasikini haukumalizika, bado uliendelea
kututafuta. Sikuwahi kupewa fedha ya matumizi
kwenda nayo shuleni, katika maisha yangu ya
shule sikuwahi kupanda daladala, ile shilingi mia
mbili ambayo nilitakiwa kupewa, mama alikuwa
akininunulia vitafunio kila niliporudi nyumbani na
kunywa chai.
SOFIA: Ilikuwaje huko shuleni?
PHIZA; Nilipata marafiki wengi sana, rafiki
mmojawapo alikuwa huyu Stellah Kimario.
SOFIA: Huyu Stellah Miss Tanzania?
PHIZA: Ndiyo huyohuyo.
SOFIA: Kwanza nilisikia kwamba ulikuwa ukitoka
naye kimapenzi, ni kweli?
PHIZA: (anamwangalia Sofia na kuanza kutoa
kicheko cha chini) Wakati mwingine ni fununu tu,
unaweza kuziamini fununu au kuachana nazo. Ila
nilimchukulia Stellah kama rafiki yangu mkubwa,
SOFIA: Tuendelee, ilikuwaje?
PHIZA: Kati ya wanafunzi ambao wazazi wao
walikuwa na uwezo, basi naweza kusema kwamba
Stellah alikuwa wa kwanza. Nilimuogopa sana kwa
kuwa alitoka familia bora, cha kushangaza, huyu
Stellah akaja kuwa karibu na mimi mno. Kumbuka
hapo tupo darasa la tano. Kila alichokuwa
akinunua, alinipatia na mimi. Sikuwahi kupewa
hela ya matumizi lakini huwezi amini, Stellah
alinifanya kushiba shuleni.
Wakati huyo masikini mimi nilikuwa na sare moja
tu ya shule, bukta imechanika matakoni na kuweka
kiraka huku shati likiwa limechanika maeneo ya
makwapani, sikujali japokuwa nilijisikia sana aibu.
SOFIA: Stellah hakuiona hali hiyo?
PHIZA: Aliiona lakini angefanya nini? Alitamani
kunisaidia lakini nahisi ilikuwa ngumu kufanya
hivyo. Ninajivunia Stellah, alikuwa akipenda kuwa
mwanamitindo toka zamani. Mara kibao alipokuwa
akibaki darasani peke yake, alikuwa akiniita na
kuniambia nimwangalie jinsi alivyokuwa akitembea
kwa maringo huku mkono wake mmoja ukiwa
kiunoni. Alipendeza sana na nilivutiwa naye mno,
ila kumwambia kwamba nampenda, lilikuwa suala
gumu sana.
SOFIA: Kwa hiyo hukuwahi kumwambia ukweli?
PHIZA: Hahaha! Mbona unakuwa na presha Sofia?
Subiri.
SOFIA: Sawa, nakuwa mpole, tiririka mwanaume.
PHIZA: Daah! Stellah!
Je, unajua nini kiliendelea kati ya Phiza na Stellah?
Tukutane Jumatano mahali hapahapa.

No comments

Powered by Blogger.